NEWS

Sunday 25 December 2022

Sikukuu ya Krismasi: Barrick North Mara yagawa msaada wa vyakula kwa vituo vya kulea watoto Tarime



Na Mara Online News
-----------------------------------

KAMPUNI ya Barrick kupitia mgodi wake wa North Mara, imevipatia vituo vya kulea watoto vya Angel House na City of Hope msaada wa vyakula na vinywaji mbalimbali kwa ajili ya Sikukuu ya Krismasi kuelekea Mwaka Mpya.

Msaada huo umehusisha mchele, unga wa ngano, mafuta ya kula, sukari, mharage, unga wa mahindi, chumvi, maji, soda, biskuti na pipi kwa kila kituo.

“Tumeona tushirikiane na watoto wanaopata malezi katika vituo hivi kufurahia Sikukuu hii ya Krismasi kuelekea mwaka mpya kupitia msaada huu mdogo,” amesema Afisa Mahusiano wa Barrick North Mara, Zachayo Makobero wakati akikabidhi msaada huo katika kituo cha Angel House Children’s Home, leo Desemba 25, 2022.

Mkurugenzi wa Angel House, James Masero (kushoto), Afisa Mahusiano wa Barrick North Mara, Zachayo Makobero (kulia) na watoto - katika picha ya pamoja wakati wa makabidhiano hayo.

Makobero amesema msaada huyo ni mwendelezo wa miingine kadhaa iliyokwishatolewa na Barrick North Mara kuchangia malezi ya watoto katika vituo hivyo.

Ametumia nafasi hiyo pia kuwatia moyo watoto waliopo katika vituo hivyo kusoma kwa bidii, huku wakimtanguliza Mungu ili hatimaye waweze kufikia ndoto zao za elimu.

Mkurugenzi wa Angel House Children’s Home, James Masero ameishukuru Barrick North Mara akisema msaada huo umewapunguzia pengo la mahitaji ya vyakula na vinywaji kwa ajili ya matumizi ya watoto kituoni hapo.

Naye Neema Mwita, akizungumza kwa niaba ya watoto wenzake wanaopata malezi katika kituo hicho, ameishukuru kampuni hiyo akisema wamepokea msaada huo kwa furaha kubwa.

“Tunawashukuru sana Barrick kwa moyo huu wa upendo mliotuonesha, Mungu awabariki na pale mlipotoa makapu yenu yazidi kufurika,” amesema Neema ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza.

Kwa upande wa City of Hope, Mkurugenzi wake, Hudson Mahare na watoto Dau Moher na Daniel Yusuf wameishukuru Barrick North Mara kwa mwendelezo wa kupeleka misaada muhimu kituoni hapo.


“Msaada huu unonesha upendo wenu [Barrick North Mara] kwetu, tunasema asanteni sana na Mungu awabariki sana,” amesema Daniel wa City of Hope.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime, unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages