NEWS

Monday 5 December 2022

Vijana 548 wahitimu fani mbalimbali Professor Mwera Foundation



Na Mwandishi Wetu, Tarime
------------------------------------------

VIJANA 548 wamehitimu mafunzo ya fani mbalimbali mwaka huu (2022), katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime (Tarime Vocational Training College), kinachomilikiwa na Taasisi ya Professor Mwera Foundation (PMF).

Mahafali ya wahitimu hao (wanaume 333 na wanawake 215) yalifanyika chuoni hapo wiki iliyopita, ambapo mgeni rasmi aliwakilishwa na Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya ya Tarime, Malema Solo.

Fani walizohitimu ni pamoja na ufundi magari, uchomeleaji, udereva, ICT, kompyuta, ukatibu muhtasi, usimamizi wa hoteli na utalii, usaidizi katika maabara na uendeshaji biashara.

Akizungumza wakati wa mahafali hayo, Mkurugenzi wa Taasisi ya PMF, Hezbon Peter Mwera alisema elimu ya mafunzo ya ufundi inawasaidia vijana kuajiriwa na kujiajiri.

“Ninawapongeza wazazi kwa kutambua umuhimu wa elimu na kupeleka vijana wao vyuoni kupata mafunzo ya ufundi,” alisema Hezbon ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Kanda ya Ziwa.

Alisema Taasisi ya PMF imeendelea kuboresha mazingira ya utoaji elimu na mafunzo ya ufundi kwa vijana ili kuwaandaa kuwa na mchango muhimu katika maendeleo ya jamii na taifa.

Alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito wa kuhamasisha watu wengine kuwekeza kwenye vyuo vya mafunzo ya ufundi ili kuwezesha vijana wengi kunufaika na fursa hiyo.

Awali, Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime, Mwalimu Frank Joash alisema chuo hicho bado kinahitaji maji ya uhakika, kompyuta zaidi na nishati mbadala (jenereta na taa za sola).

Mbali na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime, Taasisi ya PMF inamiliki Shule ya Sekondari Mchanganyiko ya wasichana na wavulana, nje kidogo ya mji wa Tarime.

Chanzo: SAUTI YA MARA

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages