NEWS

Monday 16 January 2023

Agizo la Waziri wa Kilimo: WAMACU mfano wa kuigwa


Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.

Na Mwandishi Wetu
------------------------------

AGIZO la Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe la kuvitaka Vyama Vikuu vya Ushirika kuanza kusimamia usambazaji wa mbolea kwa wakulima, limeakisi moja kwa moja utaratibu unaoendelea katika Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Mara (WAMACU LTD).

Waziri Bashe ametoa agizo hilo jana akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma, ambapo aliviagiza Vyama Vikuu vya Ushirika nchini kuanza kusimamia, kuratibu upatikanaji na usambazaji wa mbolea za mazao mbalimbali kwa wanachama na wakulima kwa ujumla.

“Kuanzia mwakani nataka kuona vyama hivi vinaratibu upatikanaji wa mbolea za mazao mengine ili wakulima waweze kupata mbolea kwa wakati na kwa urahisi kisha kuongeza tija katika uzalishaji,” amesema Waziri Bashe.

Aidha, Waziri huyo mwenye dhamana y kilimo Tanzania, ameziagiza Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kufanya kazi kwa kushirikiana na kuhakikisha mbolea inawafikia wakulima kupitia Vyama vya Ushirika.

“Mkifanikiwa kupitishia Mbolea katika Vyama Vikuu sitegemei kusikia kelele kutoka kwa wakulima kuhusu mbolea na wakati Tume ya Maendeleo ya Ushirika mmesambaa kila mikoa,” Waziri Bashe amesisitiza.

Tayari WAMACU LTD ilishaanza kusambaza kwa wakulima mbolea ya ruzuku aina ya DAP na UREA, kwa kushirikiana na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) na TFRA tangu Novemba mwaka jana.

Afisa wa CPB, Peter Mobe ndiye aliyeisaidia WAMACU LTD hadi ikafanikiwa kupata fursa hiyo ya kusambaza mbolea ya ruzuku kwa wakulima mkoani Mara.


Tangu wakati huo, Meneja Mkuu wa WAMACU LTD, Samwel Gisiboye ameendelea kutoa wito wa kuwahimiza wakulima kuchangamkia ununuzi wa mbolea hiyo iliyotolewa na Serikali kwa bei nafuu ya Sh 70,000 kwa kilo 50.

“Wakulima wajisajili kwa wingi ili kupata mbolea hii, hii ni fursa, Serikali imedhamiria kum- support mkulima,” anasema Gisiboye.

Ni dhahiri kuwa ushirika wa WAMACU LTD umeonesha mfano wa kuigwa katika suala la kuratibu, kusimamia na kusambaza mbolea ya ruzuku kwa wakulima.

"Tunahudumia mkoa kwa maana ya Tarime TC, Tarime DC, Rorya, Bunda na Butiama. Pia kwa awamu hii tunategemea kuwa na maghala ya mbolea Musoma DC na Serengeti ili kukamilisha mkoa mzima. Kwa hiyo suala hili ni la kimkoa na linaratibiwa pia na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara," anasema Gisiboye.

Meneja Mkuu wa WAMACU LTD, Samwel Gisiboye.

Menaja huyo anaendelea kuwakumbusha wakulima wanaohitaji mbolea ya ruzuku kuhakikisha wanasajiliwa na maofisa watendaji wa kata na kilimo ili kupata huduma hiyo kirahisi.

Utaratibu wa kusambaza mbolea kupitia Vyama Vikuu vya Ushirika, ikiwemo WAMACU LTD unasaidia kupunguza usumbufu kwa mkulima mmoja mmoja kuifuata kwa wakala wa usambazaji, hali inayosababisha kutumia muda mwingi kwenye foleni ya ununuzi.

WAMACU LTD inajishughulisha na ukusanyaji wa kahawa kutoka kwa wakulima kwa ajili ya kuiongezea thamani na kuitafutia masoko ya nje. Pia kwa sasa ina leseni ya uwakala wa kusambaza pembejeo ikiwemo mbolea kutoka TFRA.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages