NEWS

Monday, 30 January 2023

Bukira Sekondari: Mfano wa mageuzi makubwa sekta ya elimu Tarime Vijijini



Na Mwandishi Wetu
--------------------------------

UKIFIKA Shule ya Sekondari mpya ya Bukira, utavutiwa na kila kitu kwani vyote ni vipya - kuanzia majengo hadi wanafunzi. Ni shule ya kisasa iliyojengwa katika kata ya Sirari wilayani Tarime, kilomita chache kutoka mpaka wa Tanzania na nchi jirani ya Kenya.

Tayari shule hiyo imepokea wanafunzi 80, usawa wa jinsia ukiwa ni 50 kwa 50, yaani wasichana 40 na wavulana 40.

Wanafunzi hao ni kati ya mamia ya waliokuwa wamechaguliwa kuanza kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Sirari mwaka huu.

“Nimepokea wanafunzi 776 wa kidato cha kwanza kwa mwaka huu wa 2023, na kati ya hao, wanafunzi 80 wamehamishiwa kwenye Shule ya Sekondari mpya ya Bukira,” alisema Mkuu wa Shule ya Sekondari Sirari, Mwalimu Bulogo Mbeba katika mahojiano na Sauti ya Mara, juzi.

Kwa mujibu wa Mwalimu Mbeba, tayari wanafunzi hao 80 wameanza masomo kwa kasi katika Sekondri mpya ya Bukira.

“Bukira Sekondari ina mikondo miwili na tayari ina walimu watano na masomo yanaendelea,” anafafanua.

Ujenzi wa shule hiyo umegharimu shilingi milioni 470 zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha elimu nchini - zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan.

Gazeti hili lilitembelea shule hiyo wiki iliyopita na kushuhudia wanafunzi hao wakiwa katika vipindi vya masomo, likiwemo Hisabati.

“Huwezi kutaja mageuzi makubwa yanayonendelea katika sekta elimu ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) bila kutaja hii Shule mpya ya Sekondari Bukira, ina majengo mazuri na ya kisasa. Serikali inafanya kazi kubwa na nzuri kwenye sekta ya elimu. Miradi ni mingi kila kona,” anasema John Marwa, mkazi wa kata ya Sirari.

Shule hiyo ina vyumba vinane vya madarasa, jengo la utawala, ICT, maktaba, vyoo vya wasichana na wavulana na maabara tatu za kemia, fikia na baiolojia.

Shule hiyo imejengwa ndani ya miezi sita, alisema Mwalimu Mbeba.

Faida za shule hii
Kwa mujibu wa Mwalimu Mbeba, ujenzi wa Shule ya Sekondari Bukira umesaidia kupungunza msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Sirari ambayo hivi sasa inahudumia wanafunzi zaidi ya 1,500 wa kidato cha kwanza hadi cha nne.

“Mbali na kupungunza msongamano, imewapunguzia baadhi ya wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu kwenda na kutoka masomoni,” anaongeza Mwalimu Mbeba ambaye anatajwa kuwa mmoja wa wakuu wa shule mahiri wanaosimamia miradi ya serikali bila ubabaishaji.

Anasema ujenzi wa shule hiyo umeonesha mafanikio makubwa kutokana na ushirikiano mzuri kati ya Kamati ya Ujenzi na viongozi wa Halmashauri na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime.

Viongozi mbalimbali wakiwemo wa kitaifa wameshatembelea shule hiyo na kueleza kuridhishwa na jinsi ujenzi wake ulivyokwenda kwa kasi bila kukwama na kwa viwango vya ubora.

Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt Festo Dugange ni miongoni mwa viongozi waliozuru shuleni hapo wiki chache zilizopita na kuipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Tarime chini wa Mkurugeni wake, Solomon Shati kwa usimamizi mzuri uliofanikisha ujenzi wa shule hiyo kwa wakati.

Dkt Dugange ambaye katika ziara hiyo alifuatana na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara na viongozi wengine, pia alieleza kuridhishwa na matumizi sahihi ya fedha katika utekelezaji wa mradi huo wa elimu, wakisema ubora wa ujenzi umezingatia thamani ya fedha.

Mbali na Bukira, Serikali Kuu pia imetoa shilingi bilioni moja ambazo zimegharimi ujenzi wa shule nyingine mpya ya kisasa katika kijiji cha Nyasaricho, itakayokuwa na wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita. Taarifa zinasema miradi hiyo yote miwili ni ya viwango vya ubora wa hali ya juu.

Chanzo: SAUTI YA MARA

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages