NEWS

Monday, 2 January 2023

Halmashauri ya Tarime Mji wakamilisha madarasa 41 na sekondari mpya 2 kwa kishindo



Na Mwandishi Wetu, Tarime
---------------------------------------------

HALMASHAURI ya Mji wa Tarime imekamilisha ujenzi wa vyumba vyote 41 vya madarasa kwa gharama ya shilingi milioni 820 zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

“Madarasa yote 41 yamekamilika kwa viwango vya juu na yapo tayari kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka huu [2023],” Mkurugeni wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Gimbana Ntavyo aliiambia Sauti ya Mara mjini hapa jana.

Hivyo wanafunzi wote 3,480 waliofaulu Mtihani wa Taifa wa Kuhitimu Elimu ya Msingi Mwaka 2022 katika halmashauri hiyo watapata nafasi ya kuanza elimu ya sekondari kwa awamu moja, hakutakuwa na awamu ya pili, yaani ‘second selection’.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Ntavyo, idadi ya wasichana waliofaulu mtihani huo katika halmashauri hiyo ni 1,811 na wavulana ni 1,659, ambapo waliochaguliwa kwenda shule za bweni ni 13, wakiwemo wavulana10 na wasichana watu.

Hiyo ina maana kwamba wanafunzi wengine wote 3,467 watajiunga na shule za sekondari mbalimbali zilizopo katika halmashauri hiyo bila kuchelewa.

“Natoa wito kwa wazazi na walezi kuwafanyia watoto waliofaulu maandalizi ili wawe tayari kuingia kidato cha kwanza. Maandalizi ni mahitaji muhimu kama vile sare, madaftari na kupima afya,” alisema Mkurugenzi Ntavyo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Trime, Gimbana Ntavyo.

Mkurugenzi huyo alimshukuru Mhe. Rais Dkt Samia kwa kuipatia halmashauri hiyo shilingi milioni 820 ambazo alisema zimefanya kazi nzuri kuliko matarajio yaliyokuwepo.

“Tunamshukuru Rais wetu Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia pesa na sasa wanafunzi wote waliofaulu wataingia kidato cha kwanza kwa awamu moja,” alisema Ntavyo.

Mbali na ujenzi wa vyumba vya madarasa hayo, tumefanikiwa kupata shule mpya mbili za sekondari na hii itasaidia kuwapunguzia wanafunzi umbali wa kutembea wa hadi kilometa tano, aliongeza mkurugenzi huyo.

Alitaja shule hizo mpya kuwa ni Ikoro iliyojengwa katika kata ya Turwa na Magena katani Nkende - jirani na Uwanja wa Ndege wa Tarime (airstrip).


Ntavyo alifafanua kuwa pamoja na miundombinu mingine, halmashauri hiyo imejenga vyumba vya madarsa 10 katika shule ya Ikoro na kukamilisha ujenzi wa vyumba vinane vya madarasa na ofisi nne za walimu katika Shule ya Sekondari Magena.

Alisema Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, Michael Kembaki ameongeza nguvu katika shule hizo mpya baada ya kuzipatia shilingi milioni 3.4 kila moja kwa ajili ya ujenzi wa vyoo - kuunga mkono juhudi za wananchi.

“Mheshimiwa Mbunge kupitia Mfuko wa Jimbo amechangia shilingi milioni 3.4 kwa kila shule kuongeza nguvu ya ujenzi wa vyoo katika kila shule,” alisema Ntavyo.

Alisema ujenzi wa shule hizo mpya ni habari njema kwa wazazi na wanafunzi wa wa maeneo hayo kwa kuwa zitawaondolea adha ya kutembea umbali mrefu.

Wananchi wa mtaa wa Magena wanasema hawatausahau msaada ambao Serikali imetoa kukamilisha ujenzi wa vyumba vinane vya madarsa na ofisi mbili za walimu katika shule ambayo walianzisha ujenzi wake kwa nguvu zao wenyewe.

“Tunashukuru sana Serikali ya Mama Samia. Kwa kutuwezesha kukamilisha shule yetu na tunatarajia watoto 192 kuanza kusoma katika shule hii mapema mwaka huu,” alisema Alphonce Mang’enyi ambaye ni mmoja wakazi wa Magena.

Mang’enyi alisema shule hiyo ikakuwa ni msaada na mkombozi mkubwa kwa wanafunzi wanaohitimu elimu katika shule za msingi za Magena, Kemairi na Nyamwino.

“Ombi letu kubwa ni usajili ufanyike haraka ili watoto waingie kidato cha kwanza katika shule yetu hii mpya ya Magena,” alisema Mang’enyi ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya ujenzi wa shule hiyo.


Kwa upande wake Diwani wa Viti Maalum wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Nuru Hondy alisema ujenzi wa vyumba vya madarsa na shule hizo mpya ulienda kama uliovyopangwa na kwa kasi kubwa.

“Kazi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika halmashauri yetu ulienda vizuri na kwa kasi. Tunaishukuru sana Serikali yetu kwani kitendo cha kutupatia fedha za kugharimia ujenzi wa shule mpya ya Ikoro utasaidia sana kukabiliana na wingi wa wanafunzi katika eneo la Rebu. Rebu ni sehemu inakuwa kwa kazi sana na watu ni wengi sana,” alisema diwani huyo wa viti maalum kutoka chama tawala - CCM.

Shule mpya ya Ikoo inaifanya kata Turwa kuwa na shule tatu za sekondari za Serikali. Nyingine ni Rebu na Turwa.

Hali kadhalika kata ya Nkende nayo inaenda kuwa na shule tatu za sekondari ambazo ni Gicheri, Magena na Nkende.

Chanzo: SAUTI YA MARA

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages