NEWS

Thursday 19 January 2023

Huduma ya maji ya bomba kurejea ButiamaNa Mwandishi Wetu
-----------------------------------

BAADA ya kukosa huduma ya maji ya bomba kwa siku kadhaa, sasa baadhi ya wanavijiji katika jimbo la Butiama mkoani Mara, wataanza kupata huduma hiyo wakati wowote kuanzia leo, imeelezwa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji (MD) wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mugango – Kiabakari (MKWSSA), Mhandisi Cosmas Sanda, changamoto ya umeme iliyosababisha mamia ya wananchi hao kukosa huduma ya maji ya bomba, sasa imetatuliwa.

Mhandisi Sanda ameimbia Mara Online News mapema leo kuwa Wizara ya Maji imelipa bili ya umeme ambao ulikatwa na kusababisha huduma ya maji ya bomba kukosekana katika eneo hilo.

“Tayari umeme umesharudishwa ila kuna matengenezo yanaendelea kwenye bomba kuu na leo kazi ikikamilika mapema tunawasha na maeneo ya Mugango hadi Kiabakari yataanza kupata huduma ya maji,” alisema Mhandisi Sanda.

Hivi karibuni, Mbunge wa Butiama, Jumanne Sagini alikaririwa kwenye vyombo vya habari akikiri kuwepo kwa changamoto kubwa ya maji kwa wananchi wa Butiama, baada ya Shirika la Taifa Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) kuikatia MKWSSA nishati hiyo.

Mbunge huyo kutoka chama tawala - CCM pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages