NEWS

Monday 2 January 2023

Mbunge Waitara alivyowaumbua waongo, wanaosaka umaarufu wa kisiasa ulipaji fidia Komarera


Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara kihutubia mkutano wa hadhara kijijini Nyamwaga, wiki iliyopita. (Picha na Ernest Makanya)

Na Mwandishi Wetu, Tarime
--------------------------------------------

MBUNGE wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara amesisitiza kuwa kamwe hawezi kutetea uongo unaochochewa na watu wanaojaribu kutumia suala la uvunjaji wa nyumba katika eneo la Komarera kutafuta umaarufu wa kisiasa.

Alitangaza msimamo wake huo wakati akihutubia mkutano wa hadhara kijijini Nyamwaga wiki iliyopita, ikiwa ni siku chache tangu kuanza kwa ubomoaji wa nyumba za watu waliolipwa fidia ili kupisha upanuzi wa shughuli za Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania - kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

“Mimi ambacho nilikataa ni mambo ya uongo, mimi najua kuna maisha zaidi ya ubunge, leo mimi ni mbunge kesho sitakuwa mbunge. Kwa hiyo huwezi kunichafua kisiasa. Ukiona nimeingilia jambo ujue nimejiridhisha pasipo shaka kwamba hili - iwe mtu anachukia, iwe analia damu, iwe anagalagala - ni la kweli.

“Utaratibu wa Mbunge anayeitwa Mwita Mwikwabe Waitara, yaani mimi, nikikwambia jambo hili hapana usiendelee, ukiendelea kwa gharama zako usinitaje, na ukinitaja nitakupinga na siwezi kukutetea,” alisema Mbunge Waitara.

Alikuwa akizungumzia taarifa zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikimtuhumu kwamba ameshindwa kutetea watu waliohamishwa katika eneo la Komarera kupisha upanuzi wa shughuli za mgodi wa North Mara.

“Nimeona clip wanasema mbunge hajawatetea, amenunuliwa, mbunge amehongwa. Iko hivi, hakuna jambo ambalo nimelifuatilia kwa karibu kama hapo Komarera,” alisema Mbunge Waitara na kuendelea:

“Niliitisha mkutano pale nikawambia mnafanyiwa tathmini, kama hujaridhika na malipo yako usisaini na usichukue pesa, niliwambia mchana kweupe - haujaridhika na malipo usipokee pesa na usisaini, na nikawambia ukipokea pesa ya watu umesaini maana yake umekubali mkataba, kitakachofuata ni utekelezaji.

“Nilipoondoka wakasema mbunge anatuzuia kuchukua hela… atuache tuamue wenyewe. Nikarudi tena nikawambia nimewasikia - sikio la kufa halisikii dawa, mimi nimetimiza wajibu wa kuwambia utaratibu wa kisheria.”

Waitara ambaye ni mbunge kwa tiketi ya chama tawala - CCM, alitumia nafasi hiyo pia kuwatupia lawama baadhi ya wanasiasa akiwahusisha na mgogoro unaotengenezwa dhidi ya mgodi wa North Mara na Serikali.

“Hapa kwenye mgodi wa North Mara, (akimtaja mwanasiasa kwa jina) alikuja hapa akawambia nendeni vijana na pikipiki mkachukue mawe, uongo au kweli? (wananchi: kweli). Milipewa mawe? (wananchi: hapana). Watu walipigwa, pikipiki zikapotea, watu wakapata ulemavu na (huyo mwanasiasa) akasepa akaenda kujenga Mwanza.

“Alienda kule Nyanungu akawambia nyie nendeni mkachunge kule, watu wakapeleka ng’ombe (hifadhini) zilikamatwa, watu wakaumizwa mpaka kesho na akasepa,” alidai Mbunge huyo wa Tarime Vijijini.

Alisema baadhi ya watu wamekiuka taratibu na makubaliano yaliyofikiwa wakati Serikali inafanya uthaminishaji wa ardhi, majengo na mazao mbalimbali kwa ajili ya kulipa wananchi fidia za mali zao ili waondoke eneo la Komarera.

“Kuna mambo mengi na vituko vingi huko Komarera, wanaofanya uthamini ni Serikali, kila mtu aliitwa kwenye eneo lake akasimama akapigwa picha akaambiwa bei akakubali na kusaini akapokea pesa, na ndio maana hao watu wameogopa kuja kwangu kwa sababu wanajua mimi najua ukweli.

“Nimeongea nao mara kadhaa nikawashauri kama ndugu zungu, kwa hiyo hao wanapaswa kuondoka… Huwezi kushinda kesi mahali popote, umechukua pesa za watu umesaini, umetumia waachie eneo lao wafanye kile ambacho wamekusudia,” alisema Mbunge Waitara.

Alisisitiza kuwa watu wanaolalamika kubomolewa nyumba katika eneo la Komarera ni ambao walijenga baada ya zuio la kuendeleza chochote katika eneo la Komarera.

“Nyumba zinazolipwa pale ni ambazo zilikutwa zipo kabla ya zuio. Wengi ambao wanalalamika wamelipwa kisha wameenda wamejenga. Kwa wale ambao wamebomolewa ni waliojenga nje ya muda na siyo jambo la mbunge wala diwani, ni la kisheria. Waliopeleka kesi mahakamani kwamba nyumba zao zimebomolewa kesi haijaisha - hao kama wapo ndio waje tuwasikilize, mlango uko wazi.
Wananchi wakimsikiliza Mbunge Waitara mkutanoni kijijini Nyamwaga

Mwenyekiti wa Kijiji atoboa siri
Awali, akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Komarera, Nyamaganya Marwa alimueleza Mbunge Waitara kwamba baadhi ya watu akiwemo mama aliyemtaja kuwa siyo mkazi wa kijiji hicho wamekuwa wakitumika kupotosha ukweli wa kinachoendelea katika eneo hilo.

“Ni mwananchi [mkazi] wa Kimusi ambaye ni mama mtu-mzima, amelia sana kwenye media (vyombo vya habari) anasema mkono umekatika. Mheshimiwa Mbunge, yule mama ana mikono yote lakini anadanganya umma na akiwa na mawakala wake kwamba anaishi pale miaka yote.

“Anaonesha nyumba za watu wengine kwamba ni za kwake, hamna cha nyumba yake pale. Mwaka 2010 huyu mama aliwahi kuzua taharuki ya namna hiyo kwenye zoezi la uthamini nikiwa mwenyekiti wa kitongoji. Kuna eneo lilifanyiwa uthamini na mgodi halafu wakachelewa kufyeka mazao huyu mama akaenda akajipandia makatani pale.

“Lilipokuja zoezi la pili mgodi unataka kusogea mama akasema shamba la kwake, alilala chini akagalagala akajifanya amefariki ili akanyagwe na gari apate fidia. Huyu mama ni mwigizaji mzuri wa kuonekana ameonewa,” alisema Mwenyekiti Nyamaganya.

Baada ya maelezo hayo ya Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Komarera, Mbunge Waitara alieleza kukerwa na watu wanaopotosha umma kuhusu ukweli na kutaka kugeuza suala la Komarera kuwa la kisiasa.

“Kilichoniudhi kwa kweli ni kitendo cha watu kudanganya kwenye clip. Badala ya kutafuta haki mmeigeuza kuwa siasa na ni siasa ya CHADEMA na CCM. Tufanye kazi kwa kuheshimiana na kwa kushirikishana,” alisema Mbunge Waitara ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri katika wizara mbalimbali miaka michache iliyopita.

Wananchi wampongeza Waitara
Muda mfupi baada ya Mbunge Waitara kuhutubia mkutano huo kijijini Nyamwaga, wananchi mbalimbali - wengine kupitia kwenye mitandao ya kijamii, walijitokeza kumpongeza kwa kutangaza msimamo wake wa ukweli na uwazi kuhusu kinachoendelea katika eneo la Komarera.

“Safi sana jembe, kama kuna mtu haelewi jambo hili limekaaje basi kwa kupitia ufafanuzi huu ninaamini tumeelewa vizuri kabisa, tusipotoshe ukweli jamani, Mungu tuponye kabisa.

“Hongera sana Mhe. Mbunge Waitara kwa ufafanuzi makini kabisa maana suala hili lilikuwa limeleta sintofahamu kubwa sana, na likageuzwa kuwa la kisiasa,” mmoja wa wananchi aliandika kwenye mtandao wa kijamii.

Chanzo: SAUTI YA MARA

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages