Na Mwandishi Wetu
-------------------------------
HATIMAYE mazao ya mradi mpya wa kilimo biashara uliowezeshwa na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), yameanza kuvunwa na kupata soko kubwa.
Mgodi huo upo eneo la Nyamongo katika wilaya ya Tarime mkoani Mara, ukiendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania, kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
Mradi huo wa kilimo biashara cha umwagiliaji ulianzishwa Oktoba 2022 ili kuwezesha vijana wanaoishi katika vijiji vilivyo jirani na mgodi huo kunufaika na fursa hiyo ya kiuchumi.
Vijana 100 wa kiume na kike waliwezeshwa kuanzisha uzalishaji wa mbogamboga na matunda kwenye shamba lenye ukubwa wa ekari 10 katika kijiji cha Matongo - ambacho ni miongoni mwa vijiji 11 vya kata tano zinazozunguka mgodi huo.
Mazao yaliyoanza kuzalishwa katika shamba hilo ni pamoja na nyanya, karoti, spinachi, kabeji, sukuma wiki, chainizi, bamia, pilipili hoho na matango.
Elard Didas ni Bwana Shamba wa Taasisi ya TAHA (Tanzania Horticultural Association) katika mikoa ya Simiyu na Mara, anayetoa ushauri wa kitaalamu katika mradi huo. Anasema awamu ya kwanza ya mavuno ya mazao hayo imeanza na kuwavuta wateja wengi.
“Tumenza mavuno, mazao yote ya mbogamboga na matunda yanaenda [yananuliwa] sana. Shamba sasa hivi limekuwa kama mnada, yaani ukija huku asubuhi, mchana na jioni watu ni wengi. Tunapata walanguzi wengi na wale wa kuchukua kidogo kidogo kwa ajili ya matumizi ya nyumbani,” anasema Didas katika mazungumzo na Sauti ya Mara, juzi.
Didas anabainisha kuwa mazao hayo yanaendelea kupata soko katika mgodi wa Barrick North Mara, masoko na minada mbalimbali ya wilayani Tarime na mkoa jirani wa Mwanza.
“Masoko ni mengi, kwa mfano hizo karoti tunazipeleka Mwanza, lakini Kampuni ya AKO nao wanachukua kwa ajili ya wafanyakazi wa mgodi. Pia kuna wale wanaolisha walinzi wa mgodi nao wanachukua, lakini pia tunapeleka kuuza kwenye minada na masoko ya hapa Nyamongo na Tarime mjini,” anasema.
Mtaalamu huyo wa kilimo anatumia nafasi hiyo pia kuushukuru mgodi wa Barrick North Mara kwa kutimiza ahadi yake ya kuwa mnunuzi au soko la kwanza la mazao yanayozalishwa kwenye mradi huo wa kilimo biashara.
Anasema bado mgodi huo unaendelea ‘kuwashika mkono’ vijana wanaouendesha kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Siku ya uzinduzi wa mradi huo, Mwenyekiti wa vikundi 10 vya vijana wanaouendesha, Chacha Samson, alisema wengi wamehamasika kujiunga nao - wakiamini kuwa ni fursa muhimu ya kujipatia fedha.
“Vijana wengi wamehamasika kuchangamkia fursa hii ya fedha. Hii ni ishara kwamba miradi ya kilimo biashara katika vijiji hivi [vinavyozunguka mgodi] itasaidia pia kupunguza tatizo la vijana kuvamia na kufanya uhalifu mgodini,” alisema Samson.
Viongozi na wataalamu wanasema shamba hilo litakuwa la mfano na kwamba vikundi hivyo vitawezeshwa katika kuliendesha ili kuhamasisha vijana wengine kuchangamkia fursa hiyo ya kiuchumi.
Kwa mujibu wa Mtaalamu Mshauri kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Stanley Rubalila, kila kikundi kimepewa uhuru wa kuchagua aina ya mbogamboga na matunda yaa kulima katika shamba hilo.
Miezi michache iliyopita, Naibu Waziri wa Madini, Dkt Steven Kiruswa alizuru mgodini hapo na kupata fursa ya kwenda kujionea maendeleo ya mradi huo - ambapo alieleza kufurahishwa na hatua hiyo, akisema ni tumaini jipya kwa vijana wanaoishi maeneo hayo kupata ajira na kujiinua kiuchumi.
“Hakika moja ya njia za kunufaika na mgodi huu ni pamoja na kuanzisha uzalishaji wa bidhaa zinazohitajika mgodini, na katika hili wazalishaji wenyeji lazima wapewe kipaumbele katika uuzaji wa bidhaa wanazozalisha,” alisema Dkt Kiruswa.
Alitoa wito wa kuhamasisha vijana wanaoishi vijiji husika kutumia vizuri fursa ya uwepo wa mgodi huo - kwa kuanzisha miradi endelevu ya kiuchumi, ikiwemo ya kilimo cha mazao ya viungo, ufugaji wa ng’ombe wa nyama na kuku wa nyama na mayai.
Halmashauri ya Wilaya ya Tarime imeahidi kuunga mkono vikundi vya vijana vinavyoendesha mradi huo, ikiwa ni pamoja na kuwapatia elimu ya ujasiriamali ili kuwaimarisha katika suala la ubunifu wa fursa za kujijenga kiuchumi.
Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara aliushukuru mgodi wa Barrick North Mara kusaidia uanzishaji wa shamba hilo na kuvihimiza vikundi vya vijana vinavyouendesha kutumia kwa uaminifu fedha zilizoelekezwa kwenye utekelezaji wake ili kufikia lengo linalokusudiwa.
“Mradi huu utasaidia kujenga uhusiano wa mgodi na jamii inayouzunguka. Vijana wa maeneo haya watumie fursa hii vizuri ili kujijenga kiuchumi na uhusiano huu uendelee,” Waitara alisisitiza.
Alisema michango inayotolewa na Barrick kwa ajili ya kuboresha huduma za kijamii na kuchochea maendeleo ya wananchi kwa ujumla katika vijiji vinavyozunguka mgodi wa North Mara, imemsukuma kubadili mtazamo hasi aliokuwa nao awali dhidi ya kampuni hiyo ya uchimbaji madini.
“Kabla sijawa mbunge mtazamo wangu kwa Kampuni ya Barrick ulikuwa tofauti, lakini sasa nimeanza kuielewa,” alisema Mbunge Waitara.
Rais na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Barrick, Mark Bristow na Meneja Mkuu wa kampuni hiyo nchini Tanzania, Dkt Melkiory Ngido, wanasema uwezeshaji wa mradi huo ni sehemu tu ya michango ya kimaendeleo ambayo kampuni hiyo inaelekeza kwa jamii zinazoishi jirani na migodi yake ya dhahabu ya North Mara uliopo Tarime mkoani Mara na Bulynhulu mkoani Shinyanga.
Chanzo: SAUTI YA MARA
No comments:
Post a Comment