NEWS

Wednesday 11 January 2023

RC Mara: Kuna NGOs nyingi zinapata fedha kwa ajili ya kupinga ukeketaji Tarime lakini hatuoni mabadiliko, tuwe ‘serious’



Na Mara Online News
-----------------------------------

MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee (pichani), ameeleza kushangazwa na uwepo wa idadi kubwa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) - yanayojinasibu kupiga vita ukeketaji katika wilaya ya Tarime kwa miaka mingi sasa bila mafanikio.

RC Mzee ametoa kauli hiyo wakati alipotembelea Shirika la ATFGM Masanga wilayani Tarime jana, ambapo alionekana kukerwa na kuendelea kwa mila ya ukeketaji watoto wa kike, huku kukiwepo na NGOs nyingi zinazopata fedha kutoka kwa wafadhili kwa ajili ya kupinga vitendo hivyo vinavyotajwa kuwa vya ukatili wa kijinsia.

“Kuna NGOs nyingi zinapata fedha kwa ajili ya ukeketaji lakini hatuoni mabadiliko, imekuwa kama ni sehemu ya kupatia fedha. Suala la ukeketaji ni kama issue ya watu kufanya shughuli zao na kutajirika humo. NGOs chungu mbovu lakini ukeketaji unaendelea tu,” alisema RC Mzee.

Aliwataka waendeshaji wa NGOs hizo kuacha ubabaishaji wa kutumia mwanya huo kujipatia fedha za wafadhili na kujineemesha wenyewe, badala yake wapige vita ukeketaji kwa dhamira ya kweli ili kutokomeza tatizo hilo.

“Hawa wote wanaohusika na haya mambo ya kuzuia hili suala tuwe serious, tusiwe wababaishaji, tusidanganye kujitajirisha sisi wenyewe. Suala linazungumzwa miaka na miaka, NGOs ziko miaka na miaka, ukeketaji sasa hivi umekuwa ni wa uwazi. NGOs zinasaidia nini sasa?” alihoji kiongozi huyo wa mkoa.

RC Mzee aliendelea kuhoji, ambapo alimuuliza Meneja Miradi wa Shirika la ATFGM Masanga, Valerian Mgani akamwambia kuna NGOs saba zinazojipambanua kupinga ukeketaji wilayani Tarime.

Maswali ya RC Mzee na majibu ya Mgani yalikuwa kama ifuatavyo:
RC Mzee: Tuna NGOs ngapi zinazofuatilia suala la ukeketaji hapa Tarime?
Mgani: Ziko kama saba.
RC Mzee: Zinasaidia nini sasa, mbona ukeketaji unaendelea tu?
Mgani: (kimya).

Kisha RC Mzee aliendelea “Tufanye hizi shughuli kwa kutafuta matokeo, hatuwezi kuwa na kitu kinaendelea na sisi tunasema tunapambana, tunapambana. Tunapambanaje? Kupambana ni kitu kiishe, lakini ndio kinaongezeka… ukeketaji unaendelea.”

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Mzee ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache zimepita tangu gazeti la Sauti ya Mara lichapiche makala ya uchambuzi iliyoangazia kuendelea kwa ukeketaji licha ya kuwepo kwa 'utitiri' wa NGOs zinazopata ufadhili wa fedha kutoka mashirika ya kimataifa kwa ajili ya kutoa elimu ya kupinga vitendo hivyo wilayani Tarime.

Mkuu huyo mkoa alitumia nafasi hiyo ya kutembelea ATFGM Masanga pia kuviagiza vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi kuwakamata viongozi wa vijiji husika na wazazi wa wasichana 70 walioripotiwa kukeketwa siku chache baada ya kurudi nyumbani kwao wakitokea ATFGM Masanga walikokuwa wamekimbilia na kuishi huko kwa mwezi mzima kukwepa ukeketaji.

Haijajulikana sababu hasa ya wasichana hao kukeketwa - licha ya kuishi ATFGM Masanga inayojipambanua kutoa elimu ya kupiga vita ukeketaji.

“Taarifa tulizo nazo mpaka sasa hivi watoto 70 waliokuwa kwenye hii kambi [ATFGM Masanga] wameshakeketwa, wametoka juzi tu hapa wameshakeketwa. Lakini mbaya zaidi hakuna hata mzazi ambaye yuko kituo cha polisi mpaka sasa hivi, na taarifa tunazo na majina tunayo.

“Kwa hiyo natoa maagizo yafuatayo; majina ya watoto 70 waliokeketwa kwanza wazazi wao wote wakamatwe. Hawa wazazi wote wafikishwe mahakamani, majina tunayo na tumeshayakabidhi kwa RPC (Kamanda wa Polisi wa Mkoa). Lakini sasa hivi tunaanza kuwachulkulia hatua na viongozi.

“Mahali ambapo mtoto amekeketwa na kiongozi yupo na yeye hajachukua hatua na yeye anaingia kwenye makosa, mwenyekiti wa serikali ya mtaa naye natakiwa ashitakiwe kwanini anaacha maovu yanafanyika. “Hili jambo tulisimamie liishe na tuanze kwa kuchukua hatua,” alisisitiza RC Mzee.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages