NEWS

Wednesday 11 January 2023

RC Mzee aliomba Jeshi la Wananchi Tanzania kuwekeza Mara



Na Mwandishi Wetu, Musoma
-----------------------------------------------

MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee (pichni juu aliyesimama), amemuaomba Mkuu wa Majeshi, Jenerali Jacob John Mkunda kuangalia uwezekano wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kuwekeza zaidi katika shughuli za uzalishaji mali mkoani humo.

RC Mzee ametoa ombi hilo leo wakati Jenerali Mkunda alipotembelea ofisini kwake katika ziara yake ya kujitambulisha kwa vikosi vya jeshi vilivyopo mkoani Mara.

Ameomba jeshi hilo liwekeze kwenye kilimo cha umwagiliaji na ufugaji wa samaki.

“Mkoa wa Mara tuna eneo kubwa linalopakana na Ziwa Victoria na mito lakini hamna kilimo cha umwagiliaji na hata ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba unafanywa kwa sehemu kubwa na jeshi tu, wananchi hawajapata elimu hiyo,” alisema Mzee.

Amelipongeza JWTZ kwa kuwekeza katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba, lakini ameliomba kuongeza zaidi uwekezaji na kuwafundisha wananchi wa mkoa wa Mara kuhusiana na ufugaji wa samaki wa kitaalamu ili kuongeza uzalishaji mkoani.

Mzee ameeleza kuwa pamoja na mvua na uwepo wa Ziwa Victoria katika mkoa wa Mara, hamna kilimo cha umwagiliaji na wakulima wengi hata wanaoishi kando kando ya ziwa wanalima kwa kutegemea mvua tu, jambo ambalo alisema halileti tija.

“Hawa wananchi pamoja na elimu, lakini wanahitaji zaidi mfano waone jinsi kilimo cha umwagiliaji kinavyofayika na watapata nafasi ya kuiga, jambo ambalo linaweza kukuza uchumi wa mmoja mmoja na mkoa kwa ujumla,” amesema.

Aidha, Mkuu huyo wa mkoa ameliomba jeshi hilo kusaidia kukabiliana na uvamizi wa wavuvi katika Ziwa Victoria unaofanywa na wavamizi kutoka nchi jirani za Kenya na Uganda, jambo ambalo amesema linahatarisha maisha na kuwapa umaskini wavuvi wa Tanzania.

Kwa upande wake Jenerali Mkunda ameshukuru kwa mapokezi mazuri aliyoyapata na kuahidi kuangalia uwezekano wa JWTZ kuwekeza zaidi mkoani Mara.


Jenerali Mkunda amemtaka RC Mzee kumtumia Mkuu wa Brigedi ya Magharibi yenye Makao Makuu yake mkoani Tabora kufanikisha mipango mbalimbali ya maendeleo inayohitaji kufanywa na JWTZ katika mkoa wa Mara.

Kuhusu uvamizi wa wavuvi katika Ziwa Victoria, Mkuu huyo wa Majeshi ameahidi kuwa jeshi hilo litaendelea kulifuatilia kwa ukaribu tatizo ili kuweza kuchukua hatua stahiki kukomesha vitendo hivyo.

Mkuu wa Majeshi Jenerali Mkunda akizungumza

Aidha, Jenerali Mkunda amempongeza RC Mzee na viongozi wote wa mkoa wa Mara kwa jitihada zinazoendelea kuchukuliwa kukabiliana na mila ya ukeketaji wanawake mkoani Mara.

Hii ni mara ya kwanza kwa Mkuu wa Majeshi Jenerali Mkunda kutembelea mkoa wa Mara tangu alipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa Majeshi Tanzania, Juni 2022.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages