NEWS

Thursday, 12 January 2023

Mbunge Waitara aagiza wanakijiji Nyarwana wasomewe mapato na matumizi



Na Mara Online News
-----------------------------------

MBUNGE wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara amemwagiza Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyarwana, Elias Itembe, kuawasomea wananchi taarifa ya mapato na matumizi ya fedha walizochanga kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo ya kijijini.

Mbunge Waitara alitoa agizo hilo wakati akihutubia mkutano wa hadhara kijijini hapo jana, baada ya kudokezwa kuwa wanakijiji hawajasomewa taarifa hiyo kwa muda mrefu sasa.

Aliahidi kurudi kijijini hapo Jumamosi ijayo kusimamia usomani wa taarifa ya mapato na matumizi ya fedha zilizochangwa na wananchi.

Baadaye Mbunge huyo alikwenda kugawa godoro na vitanda vya wagonjwa na wajawazito katika zahanati za vijiji vya Wegita, Matamankwe, Pemba na Kyoruba kwa kusaidiana na Katibu Afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Sufian Mageta.

Kwa mujibu wa Mageta, hatua hiyo ni utekelezaji wa mpango wa idara ya afya chini ya usimamizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Solomon Shati.

Mbunge Waitara (wa pili kulia) wakati wa ugawaji wa vitanda na godoro

Akiwa kijijini Matamankwe, Mbunge Waitara alimpatia Mganga wa Zahanati ya kijiji hicho shilingi 50,000 za kugharimia uzalishaji wa nakala za kadi za kliniki kwa ajili ya wajawazito.

Hata hivyo alishangaa kuona zahanati hiyo ina changamoto ya kufunguliwa wakati kijiji hicho kilipewa fedha za kuikamilisha mwaka jana. Hivyo alielekeza changamoto hiyo itatuliwe haraka ili ianze kuhudumia wananchi.


Kwa upande mwingine, Mbunge Waitara ameipongeza Shule ya Sekondari Kibasuka kushika nafasi ya 10 bora katika matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Pili mwaka 2022 kwa upande wa shule za Serikari zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

Alimpatia Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Zawadi Mbunda shilingi 100,000 kwa ajili ya kuwanunulia wanafunzi husika soda.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages