NEWS

Friday 13 January 2023

RC Mzee aagiza wazazi ambao hawajapeleka watoto shule wakamatweNa Mwandishi Wetu, Bunda
-------------------------------------------------

MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee (Pichani kulia), amewaagiza Wakuu wa Wilaya zote za mkoa huo kuanza kuwachukulia hatua za kisheria wazazi wa watoto wanaotakiwa kwenda shule lakini hawajapelekwa.

RC Mzee ametoa agizo hilo jana Nyamswa wilayani Bunda, baada ya kupokea taarifa za usajili wa wanafunzi usioridhisha hadi Januari 11, 2023.

“Ninataka kuona watoto wote wamepelekwa shule au wazazi wawe wamechukuliwa hatua za kisheria na nipate taarifa ya utekelezaji wa agizo hili,” amesema.

Ameongeza kuwa haitavumilika kuona Serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya shule, ikiwa ni pamoja na kuweka walimu huku wazazi wakikwamisha jitihada hizo za kuboresha elimu nchini.

Aidha, RC Mzee amewaagiza wasimamizi wa elimu mkoani Mara kusimamia ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi wanapoenda shule.

Awali, Mkuu huyo wa mkoa aliwauliza wanafunzi wa shule za msingi mbalimbali katika tarafa ya Chamriho waliohudhuria hafla hiyo maswali ya uelewa na kutoa shilingi 10,000 kwa ambaye angeweza kujibu maswali hayo, lakini hamna aliyeweza kujibu kwa usahihi.

Amewataka Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule kuboresha mazingira ya shule na nyumba za walimu zilizopo katika mazingira ya shule ili wanafunzi waweze kujifunza sio tu masomo ya darasani lakini hata namna nzuri ya kuishi kwenye mazingira masafi.

“Mwanafunzi akija shule mbali ya masomo anajifunza kutoka kwa walimu na watu wengine wanavyovaa, wanavyoishi, wanavyoongea na wanavyofanya mambo yao, hivyo walimu wakiwa wanaishi katika mazingira ya hovyo, wanafunzi wanakuwa hawana cha kujifunza” amesema RC Mzee.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Bunda, Joshua Nassari ameeleza kuwa katika Wilaya hiyo usajiLi wa wanafunzi ni mdogo katika Halmashauri zote mbili pamoja na wilaya kuchukua hatua za kuwawezesha wazazi kuwapeleka watoto shule.

“Katika wilaya ya Bunda tumeruhusu wazazi kuwapeleka watoto shule hata wasipokuwa na sare za shule au michango ya shule ili watoto waweze kuanza masomo yao lakini bado wanafunzi wachache wameandikishwa mpaka sasa,” amesema DC Nassari.

Ametolea mfano wa kata ya Nyamswa ambapo kati ya wanafunzi 392 waliotakiwa kuanza kidato cha kwanza, niwanafunzi 90 tu walikuwa wamepokewa shuleni mpaka Januari 11, 2022.

DC Nassari ameeleza kuwa katika wilaya ya Bunda wametoa siku saba wazazi wote wenye watoto wanaotakiwa kwenda shule wawe wamepelekwa shule na baada ya hapo wataanza kuchukua hatua za kisheria.

Aidha, Mkuu huyo wa wilaya ameeleza kuwa katika fedha zilizotolewa mwaka 2022 za ujenzi wa madarasa, wilaya ya Bunda ilipata shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika halmashauri zake zote mbili.

“Kwa sasa wilaya ya Bunda ina madarasa ya kutosha kwa shule za sekondari na katika baadhi ya maeneo kuna ziada ya vyumba vya madarasa,” amesema.

Shule za msingi na sekondari zilifunguliwa Januari 9, 2022 na hadi sasa usajili wa wanafunzi wapya unaendelea katika shule zote nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages