NEWS

Tuesday 10 January 2023

Waziri wa Elimu amjibu REO Mara kuhusu msasa wa Kiingereza kwa wanafunzi



Na Mara Online News
------------------------------------

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda (pichani juu), amesema ameogea na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee azuie utaratibu uliokuwa umetangazwa na Afisa Elimu wa Mkoa (REO) huo, Benjamin Oganga - wa kuweka wanafunzi wa kidato cha kwanza kwenye programu maluumu ya wiki nane kupigwa msasa wa lugha ya Kiingereza.

“Kuna mkoa mmoja hapa, afisa mmoja alisema wanafunzi wetu wakiingia sekondari itabidi sasa wakajifunze lugha kabla hawajaanza masomo. Nimeongea na mkuu mkoa nikamwambia hata sisi tunaelewa hiyo changamoto, ila ile kalenda inayotolewa na Kamishna wa Elimu ifuatwe," alisema Prof Mkenda, hivi kribuni.

Ingawa Waziri Mkenda hakutaja jina na mkoa lakini hivi karibuni REO Oganga alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuanzia mwaka huu wanafunzi wa kidato cha kwanza watajifunza Kiingerza kwa muda wa wiki nane ili waweze kumudu lugha hiyo kabla ya kuanza masomo.

Waziri huyo mwenye dhamana ya elimu alinukuliwa jana kwenye vyombo vya habari akikiri kuwa changamoto ya lugha ya Kiingereza kwa wanafunzi ni kubwa lakini akashauri ubunifu mwingine utumike kwa sasa na kwamba yanahitajika mageuzi makubwa kuweka mambo sawa.

Katika taarifa yake, REO Oganga alitangaza pia kupiga marufuku wanafunzi kuzungumza lugha ya Kiswahili wanapokuwa shuleni.

REO Oganga akizungumza kikaoni

“Katika kuimarisha taaluma tumetoa maelekezo katika mkoa wa Mara, kuanzia Januari 9, 2023 wanafunzi wote ambao wataanza kidato cha kwanza, wataanza na ‘English Orientation’ kwa muda wa wiki nane na baada ya wiki nane tutajua viwango vya uelewa wa Kiingereza.

“Pia tumepiga marufuku lugha ya Kiswahili kutumika kwenye shule zetu za sekondari. Tunahitaji tuhakikishe kuwa wanafunzi wanamudu lugha ya Kiingereza kama ambavyo sera ya elimu na sheria ya elimu inavyoelekeza,” alisema Oganga.

Kwa mujibu wa REO Oganga, mkoa wa Mara umebaini kuwa wanafunzi wengi wanaanguka mitahini yao kwa kushindwa kumudu kujieleza kwa lugha ya Kiingereza.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages