NEWS

Monday 27 February 2023

Mahusiano ya wanavijiji na Barrick North Mara yaendelea kuimarika


Na Mwandishi Maalumu
---------------------------------------

MAHUSIANO kati ya mgodi wa Barrick North Mara na vijiji vilivyo jirani nao, yameendelea kuimarika katika miaka ya hivi karibuni, imeelezwa.

Hali hiyo inaweza kusaidia kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika vijiji hivyo na kuweka mazingira rafiki kwa mgodi huo kufanya uzalishaji wa dhahabu na kuleta manufaa zaidi.

Kampuni ya Barrick inaendesha Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa ubia na Serikali ya Tanzania, kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Habari njema kwa pande zote, yaani wananchi, Serikali na Kampuni ya Barrick, ni kwamba wenyeviti wa seriikali za vijjiji 11 vilivyo jirani na mgodi huo wanakiri kuwa mahusiano yao na mgodi huo kwa sasa ni mazuri kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko akizungumza katika kusanyiko la mashindano ya Kombe la Mahusiano.

Vikao vya mara kwa mara kati ya viongozi wa kijamii na mgodi huo vya kujadili maendeleo ya vijjiji hivyo, vinatajwa kuwa na mchango mkubwa katika kuboresha mahusiano hayo.

“Zamani tulikuwa hatuna hata vikao na tulikuwa hatuelewani na hata meneja mahusiano aliyekuwepo, lakini kwa sasa tunakaa vikao na mahusiano ni mazuri,” anasema Paul Bageni, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mjini Kati kilichopo katika mji mdogo wa Nyamongo.

Katika mazungumzo na Sauti ya Mara wiki iliyopita, Bageni alisema vikao hivyo vinahusisha wenyeviti na maofisa watendaji wa vijiji vyote 11, watendaji wa kata na madiwani wa kata tano vilipo vijiji hivyo, wakiwemo watatu wa viti maalum.

“Tunakaa kila mwezi na ikitokea dharura tunakaa,” anasema Bageni ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) ya Barrick katika mgodi wa North Mara.

Vikao hivyo vinajadili miradi inayotekelezwa chini ya mpango wa Uwajibikaji kwenye Huduma za Kijamii (CSR) wa Kampuni ya Barrick.

Mwenyekiti Paul Bageni

Kampuni ya Barrick imekuwa ikitenga mabilioni ya fedha kugharimia miradi ya kijamii kupitia CSR katika vijiji vinavyozunguka mgodi wa North Mara tangu mwaka 2019, ambapo kwa mara ya kwanza mwaka huo ilitenga dola za Kimarekani milioni 2.5.

Kwa sasa shilingi zaidi ya biloni tano zilizotolewa hivi kribuni zinaendelea kugharimia utekelezaji wa miradi ya huduma za kijamii vijijini.

Miradi inayopewa kipaumbele kupitia mpango huo wa CSR ipo kwenye maeneo matano; ambayo ni elimu, afya, usalama wa chakula, maji na uchumi.

Bageni anasema mabli na miradi ya CSR, sasa wanaelekeza nguvu pia katika kuanzisha miradi endelevu ya kiuchumi katika vijiji vilivyo jirani na mgodi huo, akitoa mfano wa mradi wa kilimo biashara ambao umeanzishwa katika kijiji cha Matongo chini ya ufadhili wa Kampuni ya Barrick.

“Tunajaribu kuangalia miradi ambayo itakuwa endelevu na tutaangalia kila kijiji kina fursa gani kama ule wa Matongo ambao ni mradi wa kuzalisha matunda na mbogamboga. Sasa tunatanua wigo tunaenda kwenye vijiji vingine,” anafafanua.

Kwa sasa anasema kuna mpango wa kuanzisha miradi ya kuku wa mayai na nyama, samaki na ng’ombe wa maziwa. “Tutaenda kijiji kwa kijiji,” anasisitiza Bageni.

Mariam Mkono ambaye ni Diwani wa Viti Maalum kutoka vijiji vilivyo jirani na mgodi wa North Mara, anasema kuna mabadiliko makubwa ambayo yanaonekana ikiwemo vijiji vyote 88 vya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kuanza kupa ‘cake’ ya uwepo wa mgodi huo.

Diwani Mariam Mkono

“Mbali na vikao ambavyo tunakaa kujadili miradi ya CSR, kizuri zaidi ni kuwa mbali na service levy (ushuru wa huduma) inayotolewa na mgodi, asilimia 30 ya fedha za CSR zimeanza kuelekezwa kwenye vijiji vingine ambavyo havikuwa kwenye mpango huo.

“Sasa hivi kata zote 26 na vijiji vyote 88 vinaonja matunda ya mgodi na asilimia 70 inabaki kwenye vijiji 11 vinavyozunguka mgodi,” anasema diwani huyo kutoka cha tawala - CCM.

Mariam anasema miaka ya nyuma mambo yalikuwa hayaendi lakini kwa sasa yanaenda vizuri kutokana na mahusiano mazuri yaliyopo.

“Mahusiano yetu hivi sasa na mgodi ni mazuri, siyo mabaya, kuna vitu vilikuwa haviendi lakini sasa vinaenda, tunakaa vikao vya pamoja na kuweka masuala ya miradi ya maendeleo ya wananchi sawa,” anongeza.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Kerende, Magabe Muniko anakiri kuwa mahusiano kati ya kijiji chake na vijiji jirani siyo mabaya kwa sasa, lakini anapendekeza kuongeza fursa za ajira kwa vijana za kufanya kazi katika mgodi huo.

Muniko pia anaomba mgodi huo kupanua wigo wa kazi kwa wakandarasi wazawa.

“Kampuni za wazawa zikipata kazi zitasaidia kukuza uchumi wa Nyamongo na zitaongeza fursa za ajira kwa vijana,” Muniko anaongeza.

Mwenyekiti Muniko Magabe

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyangoto, Mwalimu Mwita Msegi anasema mahusiano kati kijiji hicho yamekuwa mazuri baada ya Kampuni ya Barrick kuanza kutekeleza makubaliano mbalimbali kwa vitendo.

“Kwa sasa hivi mahusiano yetu na mgodi ni mazuri kama kwa asilimia 75 kwa sababu asilimia kubwa ya makubalino yetu na mgodi yanatekelezwa vizuri, ni mchache ambayo bado,” anasema Mwalimu Msegi.

Anatoa mfano wa miradi mikubwa iliyotekelezwa na mingine inayoendelea kutekelezwa chini ya mpango wa CSR kutoka Barrick North Mara.

“Tuna mradi wa maji wa kwanza mkubwa Nyamongo umeanza kutoa huduma kwa wananchi, madarasa na nyumba za walimu zinajengwa. Kwa kweli hii ni hatua nzuri sana. Hata mimi nafarijika kuwa ahadi zangu nyingi nilizotoa kwa wananchi, ikiwemo kumtua mama ndoo kichwani zinaelekea kutimia,” anaeleza Msegi.

Anataja miradi mingine ambayo italeta mabadiliko makubwa kuwa ni chuo cha VETA ambacho ujenzi wake unatarajia kuanza mwaka huu na ujenzi wa uzio wa Shule ya Sekondari Nyamongo.

Kingine kinachowapa raha viongozi hao ni vikao vyao na Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Kampuni ya Barrick, Mark Bristow.

“Tunakutana na Rais wa Barrick na matunda yake ni mengi, barabara zetu zinakarabtiwa na hata tunaenda kuwa na uwanja wa mpira wa kisasa,” anasema Mwalimu Msegi

Mwenyekiti Mwita Msegi

Lakini kwa upande mwingine, Mwenyekiti huyo naye anahimiza mgodi kupanua ajira kwa vijana wazawa, akisema ajira ndiyo imebakia kuwa changamoto kubwa katika eneo hilo.

“Uwazi katika utoaji wa ajira za mgodini ni muhimu sana katika kukuza mahusiano,” anashauri Mwalimu Msegi.

Bageni atoa rai
kwa wananchi
Mwenyekiti Bageni anatoa wito kwa wananchi kuendelea kudumisha mahusiano yaliyopo ili waendelee kufurahia neema ya uwepo wa mgodi huo.

“Ujumbe wangu kwa wananchi kwa sasa tuache mambo ya uhalifu kwa sasabu sasa tunashirikiana na mgodi vizuri na unatupatia matunda hata hatuendi kukamatia watu vitu ili kujenga mashule au mambo ya maendeleo. Mgodi uendele kuzalisha na sisi wananchi tupate pesa nzuri na kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo,” anasema Bageni

Pia anatoa wito wa kuhamasisha wananchi kukemea vitendo vya uvavizi didhi ya mgodi huo (intrusions), kwa faida ya pande zote mbili.

Taarifa zilizopo zinaonesha vitendo vya uvamizi katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara vimepungua pia kwa miaka ya hivi karibuni kutokana na mahusiano bora yaliyopo baina ya mgodi huo na vijiji vilivyo jirani nao.

Chanzo: SAUTI YA MARA

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages