NEWS

Thursday, 13 November 2025

Dalili za mlipuko wa homa ya nguruwe zaripotiwa Butiama



Nguruwe

Na Mwandishi Wetu

Halmashauri ya Wilaya ya Butiama mkoani Mara imetangaza kukumbwa na dalili za mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nguruwe ujulikanao kama African Swine Fever.

Tangazo kwa umma lilitolewa na ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Novemba 11, 2025, huku wataalamu wakisema ugonjwa huo hauna tiba na huenea kwa kasi baina ya nguruwe wagonjwa na wazima.

Tayari nguruwe 16 wameripotiwa kufa kati ya Novemba 10 na 13, 2025 katika maeneo tofauti ndani ya Butiama, kwa mujibu wa wataalamu wa mifugo wa halmashauri hiyo.

“Tulianza kuona dalili za ugonjwa wa homa ya nguruwe Novemba 10, 2025, ikabidi tuchukue hatua za tahadhari haraka, ikiwa ni pamoja na kuwaarifu maafisa watendaji wote wa vijiji na kata wilayani.

“Kisha tuliwajulisha viongozi wa mkoa na Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Wanyama Kanda ya Ziwa kilichopo mkoani Mwanza,” mtaalamu wa mifugo kutoka Butiama ameiambia Mara Online News kwa simu jioni hii.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, tayari uongozi wa wilaya umechukua sampuli na kuipeleka kuchunguzwa kwenye kituo hicho cha Utafiti wa Magonjwa ya Wanyama.

“Kutokana na hali hiyo, Kama Halmashauri ya Wilaya tumezuia usafirishaji, uuzaji na uchinjaji wa nguruwe na mazao yake katika halmashauri yetu,” amesema mtaalamu huyo wa mifugo ambaye hakupenda kutajwa jina.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages