NEWS

Thursday 9 February 2023

Matunda ya CSR Barrick: Mradi mkubwa waanza kusambaza majisafi na salama kwa wananchi Nyamongo


Wakazi wa kitongoji cha Minarani kijijini Nyangoto - Nyamongo wakifurahia kupata huduma ya majisafi na salama katika kimojawapo cha vituo vya mradi mkubwa uliotokana na fedha za CSR Barrick North Mara

NA Mwandishi Maalumu
-------------------------------------

UKIWATAZAMA wakati wanachota maji utakutana na nyuso zilizojaa tabasamu na furaha ya kupata huduma ya majisafi na salama. Hawa si wengine bali ni wakazi wa kijiji cha Nyangoto kilichopo kata ya Matongo, jirani na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime, Mara.

Tayari vituo kadhaa vya kutolea huduma ya maji hayo kwa wananchi vimeanza kufanya kazi katika vitongoji vyote saba vinavyounda kijiji cha Nyangoto kinachokadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya 15,000.

Vitongoji hivyo ni Minarani, Nyangoto, Nyamekoma, Mnadani, Majengo Mapya, Stooni na Lamboni.

Sehemu kubwa ya wakazi wa kijiji hiki wameanza kupata huduma ya majisafi na salama ya bomba -ambayo rangi yake inaashiria uhai kama ulivyo msemo wa “maji ni uhai”.

“Maji ni masafi ni mazuri, ninawatakia waliotuwezesha kupata huduma hii maisha mema na mafanikio mengi katika kazi zao,” anasema Elizabeth John, mmoja wa wanawake waliozungumza na gazeti hili wakiwa wanapata huduma ya maji hayo katika kituo kilichopo kitongoji cha Minarani, wiki iliyopita.

Huduma hiyo kwa sasa inatolewa kwa wananchi hao bila malipo wakati Bodi ya usimamizi wa mradi huo ikijipanga kuweka utaratibu wa kuchangia fedha kidogo.

Francisca Philipo, mkazi mwingine wa kijiji cha Nyangoto anasema ujio wa mradi huo umewaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji.

“Tulikuwa tunatembea umbali mrefu kutafuta maji ya kununua, lakini kwa sasa unatembea ndani ya dakika tano unachota maji, hii inatupa furaha sana,” anaongeza Francisca huku akionesha tabasamu kubwa.

Wananchi wakipata huduma ya maji ya mradi huo kwenye kituo cha kitongoji cha Minarani katika mji mdogo wa Nyamongo

Wananchi hao wanachoomba sasa ni huduma hiyo kusimamiwa vizuri ili iwe endelevu kwa manufaa wa kizazi cha sasa na vijavyo.

“Tunaomba viongozi wetu wasimamie huu mradi vizuri na sisi wananchi pia tuutumie vizuri ili uwe endelevu,” anasema Francisca.

Wakazi wa kijiji hicho wanasema muda waliokuwa wanatumia kutembea umbali mrefu kutafuta maji sasa watautumia kufanya shughuli nyingine za maendeleo zikiwemo za kujipatia kipato.

“Tumefurahi sana wananchi wa Nyamongo, sasa hivi unachota maji unaendelea na shughuli nyingine, siyo kama zamani ambapo tulikuwa tunatumia muda mwingi kutafuta maji,” anasema Diana Lucas, mwanadada anayejishughulisha na biashara wa M-PESA katika mji mdogo wa Nyamongo.

Mwenyekiti Kitongoji cha Minarani, Elisha Wilson Wambura anasema mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa wakazi zaidi ya 1,200 wa eneo hilo.

“Huu mradi ni wa CSR (Mpango wa Uwajibikaji kwenye Huduma za Kijamii), na maji haya ni mbadala wa vyanzo vya maji tulivyokuwa tunatumia kwenye eneo lililochukuliwa na mgodi,” anasema Elisha ambaye pia anakiri kuwa ndio mradi wa kwanza mkubwa kuwahi kujengwa katika eneo la Nyamongo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyangoto, Mwalimu Mwita Msegi, wakazi wote wa kijiji hicho wameanza kupata huduma ya majisafi na salama ya bomba kutoka kwenye mradi huo, shukrani kwa mpango wa CSR wa Kampuni ya Barrick kwa kuwezesha upatikanaji wa mradi huo uliogharimu takriban shilingi bilioni moja.

“Kijiji chote sasa kimeanza kupata huduma ya maji na huu ni mradi wa kwanza mkubwa kwa Nyamongo, na vituo vya kuchotea maji vimejengwa kwenye vitongoji vyote,” anasema mwenyekiti huo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyangoto, Mwalimu Mwita Msegi (kulia) na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Minarani, Elisha Wilson wakionesha sehemu ya miundombinu ya mradi huo. (Picha zote na Sauti ya Mara)

Mwalimu Msegi anaendelea “Lengo letu kubwa ni kwamba kila mtu apate maji ya bomba nyumbani kwake - afungiwe mita ili alipe bili kulingana na matumizi yake, siyo kwenda kuchota kwenye vituo. “Tumedhamiria kufanya hivyo ili kumtua mama ndoo ya maji kichwani - asihangaike kwenda kutafuta maji.”

Anafafanua kuwa kijiji cha Nyangoto kimekuwa cha kwanza kujengewa vituo vya kuchotea maji na wakazi wake kuanza kupata huduma hiyo kwa sababu mradi huo umejengwa kijijini hapo. “Lakini pia mradi huu umebuniwa na kijiji cha Nyangoto, ingawa kwa sasa ni wa kata ya Matongo. Lakini chimbuko la mradi huu ni kijiji cha Nyangoto,” anaongeza.

“Kwa awamu ya kwanza, tunatarajia kusambaza maji ya bomba kwa wakazi zaidi ya 30,000 katika vijiji vinvyolengwa na mradi huu, na tayari Barrick imejenga mtambo wa kusafisha maji kwa ajili ya matumizi ya wananchi,” anasema Mwalimu Msegi na kuongeza kuwa tayari imeshaundwa Bodi ya kusimamia mradi huo - itakayotekeleza majukumu yake chini ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

Mbali na Nyangoto, vijiji vingine ambavyo vitanufaika na mradi huo ni Matongo, Nyabichune na Mjini Kati.

Kuhusu hali ya ubora wa maji ya mradi huo, Mhandisi Mohamed Mtopa kutoka RUWASA Wilaya ya Tarime, anasema ni safi na salama kwa matumizi ya watu.

“Ni majisafi na salama kwa sababu tunayachukua mgodini [mgodi wa North Mara] ambapo wanayatoa mto Mara wanayatibu, baada ya hapo mengine yanaingia kwenye kambi zao na baadhi tunayapampu kuja kwenye tenki letu lenye uwezo wa kuchukua lita 300,000 kwa wakati mmoja,” anasema Mhandisi Mtopa.

Sehemu ya juu ya tenki la maji la mradi huo lenye uwezo wa kuchukua lita 300,000 kwa wakati mmoja

Mhandisi Mtopa anabainisha kuwa mradi huo utawapunguzia wakazi wa kata ya Matongo kero iliyokuwepo kwa asilimia 85, na kwamba kila mtu kwa sasa ana uhuru wa kuunganishiwa huduma ya maji ya bomba, tofauti na zamani ambapo ilikuwa lazima uende kutafuta, au kununua maji kwa wanaoyatembeza kwenye baiskeli.

“Wito wetu kama RUWASA ni kwamba wananchi tulinde miundombinu ya maji, tuepuka kukata mabomba, lakini pia tuwe wazalendo kwa kuchangia bili ya maji mradi uwe endelevu, ili hata mgodi wa North Mara ukiondoka wananchi tuweze kuendeleza mradi wetu,” anasisitiza Mhandisi Mtopa.

North Mara ni mmoja wa migodi mikubwa inayoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania, kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Mbali na kulipa kodi za serikali na kutoa ajira mbalimbali kwa Watanzania, mgodi huo unatenga mabilioni ya fedha kila mwaka kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kijamii kupitia mpango wake wa CSR.

Miradi inayopewa kipaumbele kupitia mpango wa CSR ipo kwenye maeneo matano; ambayo ni elimu, afya, usalama wa chakula, maji na uchumi.

Chanzo: SAUTI YA MARA

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages