NEWS

Monday 20 February 2023

Tete Foundation na wadau wake washusha msaada Kituo cha Hopes Disabilities, shule za kata ya Miono iliyopo Chalinze, Bagamoyo - PwaniNa Mwandishi Wetu, Chalinze
---------------------------------------------

WATOTO wenye ulemavu na wasiojiweza katika Kituo cha Hopes Disabilities kilichopo kata ya Miono, Halmashauri ya Chalinze, Bagamoyo mkoani Pwani, wamepokea msaada wa vitu mbalimbali vilivyokuwa changamoto kwao kutoka Taasisi ya Tete (Tete Foundation) kwa kushirikiana na Kampuni ya Bima ya Reliance na Benki ya DTB Tawi la Dodoma.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Februari 18, 2023, Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa Tete Foundation, Suzana Senso alisema kabla ya kufikiria kupeleka msaada huo kwenye Hopes Disabilities Centre, walifanya utafiti na kubaini kituo hicho kinahitaji kubwa kuliko vingine.

Suzana alisema baada ya kubaini changamoto hiyo aliwasiliana na Kampuni ya Bima ya Reliance Tanzania Limited na Benki ya DTB Tawi la Dodoma ambazo kwa uzalendo hazikusita kukubali ombi la kuwachangia msaada huo.


“Tunamshukuru Mungu siku ya leo ambayo imekuwa ni siku ya kipekee tukiwa tunakamilisha kampeni yetu iliyoitwa ‘Tunaamini katika wewe’ huku maeneo ya Miono, Chalinze - Bagamoyo mkoani Pwani tuliyoianzisha tarehe 9, Januari mwaka huu.

“Tunaposema tunaamini katika wewe ‘buku’ yako moja inakwenda kumgusa mtoto mmoja anayeishi katika mazingira magumu kwa kumnunulia peni au penseli.

“Tumekuwa na hii kampeni kwa karibia mwezi mmoja na nusu na leo ndiyo tumefikia kilele huku Miono. Lakini kikubwa zaidi tumeweza kuwapatia watoto hawa msaada mkubwa zaidi ya tulivyotarajia.


“Tunawashukuru wote waliojitoa kwa moyo wao wa uzalendo lakini shukrani za kipekee ziwaendee Reliance Insurance Tanzania Limited kupitia Benki ya DTB waliotuunganisha nao na kutuwezesha kutimiza lengo letu,” Suzana alisema na kuongeza:

“Pia tunawashukuru sana wale wote waliokuwa wakichanga zile elfu moja moja zao kupitia zile lipa namba zetu tulizokuwa tumeziweka kwenye mitandao ya kijamii.

“Nipende kutumia nafasi hii kumshukuru Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Reliance Insurance Tanzania Limited, Madam Rukia Goronga na msafara wake kwa kuonesha kujali zaidi na kutumia muda wao kuhudhuria tukio hili, pia Meneja wa DTB Benki Mkoa wa Dodoma ambaye ametuma mwakilishi wake baada ya kupatwa na dharura, Mungu ambariki sana.”


Suzana alitumia nafasi hiyo pia kuwasihi wananchi wengine popote walipo kuwakumbuka watoto wenye mahitaji katika maeneo mbalimbali, akisema kuna sehemu walikuta mtoto akilazimika kutumia daftari moja kuandikia masomo yote.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa Reliance Insurance, Rukia Goronga akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya msaada huo, aliipongeza kampeni hiyo na kuahidi kuwa kampuni yake itaiunga mkono kwa siku zijazo.

Naye Diwani wa Kata ya Miono na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze, Mheshimiwa Juma Ramadhani aliipongeza Tete Foundation kwa kuelekeza msaada huo kwenye kata yake na kuimbea kwa Mungu taasisi hiyo izidi kustawi na kusaidia kata hiyo na nyingine.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages