NEWS

Friday 24 February 2023

Viongozi CCM, Serikali waunguruma kikao cha mikakati ya ushirikiano kupaisha maendeleo ya mkoa wa Mara


Mjumbe wa NEC ya CCM Mkoa wa Mara, Christopher Mwita Gachuma akizungumza kikaoni.

Na Mara Online News
-----------------------------------

VIONGOZI wa ngazi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali Mkoa wa Mara, leo wamekutana wilayani Tarime kufahamiana na kuweka mikakati ya kushirikiana katika kusimamia na kutekeleza ilani ya chama hicho tawala, kwa maendeleo ya kisekta na maslahi mapana ya wananchi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla.

Kikao hicho kimeongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi, ambapo amewahimiza viongozi wa pande hizo mbili kujenga na kudumisha mshikamano katika kutekeleza majukumu yao ya kiutumishi.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi akisisitiza hoja kikaoni.

“Viongozi wa Chama na Serikali lazima tuwe wamoja ili kuhakikisha mkoa wetu unanyanyuka kimaendeleo,” Chandi amesisitiza na kuwataka wabunge wa mkoani Mara wanaotokana na CCM kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kiwango kinachokidhi mahitaji ya wananchi katika majimbo yao.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM wa Mkoa wa Mara na mwenyeji wa kikao hicho, Christopher Mwita Gachuma amekazia hoja hiyo akisema Serikali na CCM vinajenga nyumba moja ya kutekeleza ilani ya chama hicho tawala na kuwaletea wananchi maendeleo, na hivyo kukiwezesha kuendelea kushika madaraka ya nchi, ikiwa ni pamoja na kupata ushindi wa kishindo kuanzia uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 hadi uchaguzi mkuu mwaka 2025.

Wajumbe kikaoni

Naye Mjumbe wa NEC (Viti 3 UWT Tanzania Bara), Joyce Ryoba Mang'o ameongeza kuwa majukumu ya CCM na Serikali ni pamoja na kuhakikisha wananchi Watanzania wanapata maendeleo ya kisekta kwa kiwango kinachoridhisha.

Mjumbe wa NEC, Joyce Ryoba Mang'o.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee amewashukuru viongozi wa CCM kwa ushirikiano mzuri wanaompa katika kusimamia na kuhamasisha shughuli za maendeleo ya mkoa huo, lakini pia kutatua changamoto na migogoro.

Hata hivyo kwa upande mwingine, Mzee ametumia nafasi hiyo pia kukemea tabia ya wanachama wachache wanaotumia mitandao ya kijamii ikiwemo WhatsApp kushambulia kwa matusi viongozi wa CCM na Serikali.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee akizungumza kikaoni.

Kiongozi huyo wa mkoa ametaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya wanachama wanaojihusisha na vitendo hivyo, akisema ni watu wenye nia ovu ndani ya chama hicho.

“Mimi kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa, ninaagiza mamlaka husika zichukue hatua mara moja na nipate mrejesho. Watu lazima heshima iwepo kati ya wadogo kwa wakubwa, wanachama, viongozi na wananchi kwa ujumla, ndiyo miiko na desturi ya nchi yetu,” amesema.

Mbunge wa Butiama ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini naye ametaka watu wote wanatoa kauli za matusi na uchochezi wachukuliwe hatua kwenye vyombo vya dola ili kuepusha uvunjifu wa amani katika jamii.

Mbunge wa Butiama, Jumanne Sagini akichangia hoja kikaoni.

“Haiwezekani mtu anatukana na kufanya uchochezi dhidi ya wananchi, Serikali na Chama Cha Mapinduzi hachukuliwi hatua yeyote wala kuhojiwa. Tunataka tudumishe amani na mshikamano ndani ya nchi yetu,” Sagini amesisitiza.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages