NEWS

Monday 20 March 2023

Kishindo cha miaka miwili ya Mbunge Chege Rorya, atekeleza ahadi lukuki za miradi ya kisekta jimboni



Na Mwandishi Wetu
--------------------------------

KWA mara ya kwanza katika historia ya jimbo la Rorya, Jafari Wambura Chege (pichani) amekuwa Mbunge wa kwanza kufanikiwa kutekeleza idadi kubwa ya ahadi zake kwa wananchi katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake.

Hadi sasa, Mbunge Chege ambaye alipata ridhaa ya wananchi ya kuongoza jimbo hilo tangu mwaka 2020, ameweza kutekeleza ahadi nyingi za miradi ya kisekta, na hivyo kupunguza kero kwa wapigakura wake.

Mafanikio makubwa ya utekelezaji wa ahadi zake katika kipindi hicho kifupi yameonekana zaidi katika sekta za maji, elimu, afya na miundombinu ya barabara.

Maji
Ahadi alizotekeleza ndani ya jimbo la Rorya katika kipindi hicho ni pamoja na ufufuaji wa miradi ya maji Komuge, Nyarombo, Nyambori, Shirati, Nyihara, Ng’ope, Marasibora na Masonga.

“Pia niliahidi kusimamia Serikali kujenga miradi ya maji Rabour, Raranya na Kwibuse, na wakazi wa Ingri Juu kupata maji ya Ziwa Victoria, lakini pia ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji Rorya - Tarime ili kata zote 26 za jimbo la Rorya zinufaike. Ahadi zote hizi nimezitekeleza,” amesema Mbunge Chege katika mahojiano na Sauti ya Mara jimboni Rorya, wiki iliyopita.

Afya
Kwa upande wa sekta ya afya, Mbunge Chege amefanikiwa kutekeleza ahadi yake ya kuiomba Serikali kujenga Kituo cha Afya Nyancha na kingine katika tarafa ya Luo-Imbo.

“Niliahidi pia kumalizia ujenzi wa zahanati zilizojengwa kwa nguvu za wananchi, na tayari nimetekeleza ahadi hizo katika zahanati za Oliyo, Muhundwe, Osiri, Ng’ope, Dett na Makongro,” anaongeza.

Ahadi nyingine ni za kuanzisha ujenzi, au kukamilisha maboma ya zahanati katika kila kijiji, ambapo tayari Mbunge Chege ameanza na zahanati 18, ambaazo ni Kisumwa, Nyanchabakenye, Kyanyamsana, Nyihara, Irienyi, Mori, Omuga, Gabimori, Manira, Nyabikondo, Kirogo, Randa, Nyamasyeki, Mkoma, Nyahera, Tabache na Kukona.

“Lakini pia nimetekeleza ahadi ya kuboresha zahanati za Kogaja, Ikoma na Hospitali ya Wilaya,” anaongeza Mbunge Chege.


Miundombinu
“Kwenye miundombinu, niliahidi kusimamia Serikali kujenga daraja la mto Mori na mto Wamaya, nimetekeleza. Niliahidi kusimamia Serikali kujenga daraja la Kowak, nimetekeleza,” anasema Mbunge Chege.

Ahadi zake nyingine katika sekta ya miundombinu ni zile za kusimamia Serikali kujenga daraja la mto Sakawa, ambapo tayari mkandarasi yupo eneo la ujenzi, na ahadi ya kufungua barabara za kuunganisha kata na kata, kijiji na kijiji imeshatekelezwa.


Elimu
Katika jitihada za kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu kwenda na kutoka shule, Mbunge Chege aliahidi kuanzisha ujenzi wa shule mpya za sekondari katika maeneo mbalimbali.

Mbunge Chege anasema tayari ametekeleza ahadi hiyo, akitaja shule mpya za sekondari zilizojengwa kuwa ni Mkengwa, Mika, Nyang’ombe, Nyamagaro, Ikoma, Nyambogo, Changuga, Kigunga na Rwang’enyi.

Kwa mujibu wa Mbunge huyo, ujenzi wa shule hizo umehusisha vyumba vipya vya madarasa 178 kutokana na fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Anataja ahadi zake nyingine alizotekeleza kwenye sekta ya elimu kuwa ni kama ifutavyo:

Ukamilishaji wa sakafu ya maboma mawili ya madarasa, plasta na kupaka rangi katika Shule ya Sekondari Waningo na vyumba viwili vya madarasa kwa kuweka sakafu, rangi na plasta katika Shule ya Msingi Erengo.

Ununuzi wa mbao, mabati na upauaji wa maboma mawili ya madarasa katika Shule ya Msingi Kyanyamsana na ukamilishaji wa madarasa mawili kwa kuweka sakafu, plasta na rangi katika Shule ya Sekondari Nyihara.

Ukamilishaji wa madarasa mawili kwa kuweka sakafu, plasta na rangi katika Shule ya Msingi Nyihara, ukamilishaji wa zahanati ya Oliyo na vyumba viwili vya madarasa kwa kuweka plasta, sakafu, kupaka rangi pna choo cha cha wanafunzi katika Shule tarajali ya Msingi Kyaembwe.

Pia ukamilishaji wa sakafu, rangi na plasta kwenye vyumba vinne vya madarasa katika Shule ya Sekondari Nyabiwe na maboma mawili ya madarasa kwa kuweka sakafu, plasta na rangi katika Shule ya Sekondari Nyamagaro.

Ukamilishaji wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi kwa kuweka sakafu na kupaka rangi katika Shule tarajali ya Sekondari Komuge, zahanati ya kijiji cha Osiri, upauaji wa darasa katika Shule ya Msingi Nyahera na darasa katika Shule ya Msingi tarajali ya Nyakibori.

Ununuzi wa saruji mifuko 150 kwa ajili ya ujenzi wa Shule tarajali ya Sekondari Nyangombe na kuchangia maabara wa Shule ya Sekondari Nyamasanda.

Uchangiaji wa ujenzi wa matundu 12 ya choo cha wanafunzi katika Shule ya Sekondari Goribe, ukamilishaji wa darasa katika Shule tarajali ya Msingi Mauwe na ununuzi wa saruji mifuko 100 kwa ajili ya Shule ya Sekondari Mika.

Mbunge Chege akijenga hoja bungeni Dodoma

Pia Mbunge Chege aliahidi na kutekeleza uchangiaji wa vifaa katika shule za msingi na sekondari mbalimbali kama ifuatavyo:

Shule ya Msingi Manyanyi (mabati 60), Shule ya Msingi Ryagati (saruji mifuko 30), Shule ya Msingi Obolo (saruji 30) na Shule ya Sekondari Sarungi (saruji 10).

Shule za Msingi Nyahera (saruji 50), Sota (mabati 40), Rwangenyi (madawati 10), Shule ya Sekondari Nyamtinga (mabati 54), Shule za Msingi Tacho (saruji 30), Radienya (maboresho ya choo) na Chirobi (saruji 15 na maboresho ya choo).

Shule za Msingi Omuga (tenki la maji, Sudi (saruji 50), TANU Milale (mabati 54), Ingri Chini (saruji 30), Mang’ore (matofali 2,000), Mauwe (saruji 40), Tatwe (mabati 54 na ufundi), Nyihara (ujenzi wa choo), Kyanyamsana (mabati 59) na Shule ya Sekondari Changuge (saruji 50).

Shule za Msimgi Bitiryo (mabati 54), Binatso (madirisha nyumba ya mwalimu, Kibuyi (mabati 54), Kinesi (saruji 50), Kuruya (saruji 50), Mbatamo (saruji 50), Mariwa (saruji) na Shule Sekondari Komughe (mabati 70).

Nyingine ni Shule za Sekondari Kigunga (saruji 100), Kigunga (hela ya ufundi shilingi 500,000 na mawati 10), Nyambogo (mabati 108), Shule za Msingi Mbire Tai (mabati 108), Busanga na Siko (saruji 25), Bwiri saruji 100), Ochuna (saruji 60) na Shule ya Sekondari Rwangenyi (saruji 50).

Aidha katika ufuatiliaji wa fedha za Serikali ya Awamu ya Sita ili kutimiza ahadi, baada ya uchaguzi Ofisi ya Mbunge ilifanya ziara na kuchukua changamoto kwa kila shule iliyofikiwa na kuziwasilisha kwenye wizara husika serikalini.

“Shukrani za kipekee kwa Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan kwa kuzipatia baadhi ya shule zetu fedha - kiasi cha shilingi milioni 600 za mpango wa P4R,” anasema Mbunge Chege.

Anazitaja shule hizo na kiasi cha fedha zilizopata kikiwa kwenye mabano kuwa ni Shule ya Msingi Charya (Sh milioni 40 za ujenzi madarasa mawilli), Shule ya Sekondari Nyathorogo (Sh milioni 80 za ujenzi wa bweni) na Shule ya Sekondari Nyambogo (Sh milioni 40 za ujenzi wa madarasa mawili).

Nyingine ni Shule za Msingi Rayudhi (Sh milioni 40 za ujenzi madarasa mawili), Bugendi B” (Sh milioni 40 za ujenzi madarasa mawili), Obolo/ Manyanyi (Sh milioni 40 za ujenzi wa madarsa mawili) na Masara (Sh milioni 40 za ujenzi wa madarasa mawili).

Pia Shule za Msingi Kyanyamsana (Sh milioni 40 za ujenzi wa madarasa mawili) Nyamagaro (Sh milioni 40 za madarasa mawili), Shule za Sekondari Bukama (Sh milioni 80 za ujenzi wa bweni), Waningo (Sh milioni 40 za ujenzi wa madarasa mawili), Tai (Sh milioni 40 za madarasa mawili na Mirare (Sh milioni 40 za ujenzi madarasa mawili).

“Haya ni baadhi tu ya maendeleo niliyofanikiwa kuyawezesha katika jimbo langu la Rorya ndani ya kipindi cha miaka miwili ya uongozi wangu,” anahitimisha Mbunge Chege anayetokana na chama tawala - CCM.

Chanzo: SAUTI YA MARA

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages