NEWS

Monday 13 March 2023

Mjumbe Mkutano Mkuu CCM Taifa Chonchorio ahimiza nidhamu UVCCM, ataka Waitara, Kembaki, Ngicho waheshimiwe


Mjumbe wa Mkutano Mkuu CCM Taifa, Daniel Chonchorio (kulia) na Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Tarime, Godfrey Gotora wakishiriki kuimba wimbo wa chama wakati wa mkutano wa baraza la umoja huo mjini Tarime, juzi.

Na Mwandishi Wetu, Tarime
------------------------------------------

MJUMBE wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Daniel Chonchorio, amekemea kauli za matusi zinazotolewa na baadhi ya vijana na wanachama kwa viongozi wa chama hicho na serikali katika wilaya ya Tarime mkoani Mara.

“Mheshimiwa Ngicho [Daudi Marwa Ngicho] ni Mwenyekiti wetu wa chama ngazi ya wilaya, Mheshimiwa Waitara [Mwita Waitara] ni Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini na Mheshimiwa [Michael Kembaki] ni Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini. Hawa ndio viongozi waliochaguliwa na wananchi, lazima wapewe heshima yao,” Chonchorio alisisitiza katika mazungumzo na Sauti ya Mara muda mfupi baada ya kuhutubia mkutano wa Baraza la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Tarime mjini hapa, juzi.

Alisema kutoa ushauri na kukosoa viongozi sio vibaya lakini siyo kuwabeza kuwashambulia kwa matusi hadi kwenye mitandao ya kijamii.

Mjumbe huyo wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa aliwataka vijana na wanachama wanaoendekeza matusi kwa viongozi kujirekebisha na kuacha tabia hiyo mara moja, la sivyo chama hicho hakitasita kuchukulia hatua kali za kinidhamu dhidi yao.

“Vijana watakaokosa nidhamu tutawashauri na wakiendelea basi tutachukua hatua zaidi kwa sababu hakuna mkubwa zaidi ya chama,” Sauti ya Mara ilimnukuu kiongozi huyo.

Chonchorio ambaye pia ni mfanyabiashara alisisitiza kuwa viongozi wa CCM na Serikali lazima waheshimiwe na kupewa nafasi ya kutekeleza ilani ya chama hicho tawala kwa ajili ya kuharakkisha maendeleo ya wananchi.

Awali, akizungumza katika mkutno huo wa UVCCM akimwakilisha Mjumbe mwenzake wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Manchare Heche, Chonchorio aliwataka vijana wa umoja huo kudumisha nidhamu, mshikamamo na kujitolea kukitumikia chama hicho kwa vitendo.

“Tunapota nafasi hizi za chama lazima tujitolee kukitumikia chama chetu ili kisonga mbele. Nafasi hizi tumepewa kukutumikia chama kwa kujitolea na siyo mapambo,” alisema.

Katika hatua nyingine, Chonchorio aliwasilisha ahadi ya ng’ombe wawili wa maziwa kutoka Manchare huku naye akimuunga mkono kwa ahadi ya ng’ombe mmoja wa maziwa kwa ajili ya mradi wa ufugaji unaoanzishwa na UVCCM Wilaya ya Tarime.

Pia Chonchorio aliahidi kutoa msaada wa saruji mifuko mitatu, lita kumi za rangi na shilingi laki moja kwa ajili ya ukarabati wa ofisi ya UVCCM Wilaya ya Tarime ili kuifanya kuwa ya kisasa.

Katibu wa Hamasa, Chipukizi Itifaki na Mawasiliano Wilaya ya Tarime, Emmanuel Sabato alitambulishwa katika mkutano huo wa Baraza la UVCCM ambapo alitumia nafasi hiyo kuahidi kuimarisha zaidi idara ya chipukizi na kuhakikisha vijana wa chipuki wanapata haki zao za msingi, ikiwemo elimu.

Chanzo: SAUTI YA MARA

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages