Na Mwandishi Wetu
---------------------------------
UJENZI wa mizani ya kisasa ya kupima uzito wa magari huku yakiwa kwenye mwendo katika eneo la Rubana wilayani Bunda, Mara umefikia asilimia 50.6.
Hayo yalielezwa na Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TNROADS) Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe wakati Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Godfrey Kasekenya alipokwenda kukagua mradi huo, juzi.
“Utekelezaji wa mradi huo umeanza Januari mwaka huu na tayari umefika asilimia 50.6 huku ukitarajiwa kukamilika Mei mwaka huu kwa ajili ya kusaidia kupunguza msongamano wa magari na kudhibiti yanayozidisha uzito, ili kulinda na kuhifadhi ubora wa barabara,” alisema Mhandisi Maribe.
Mhandisi Maribe aliongeza kuwa mizani hiyo itakuwa na uwezo wa kupima uzito wa magari yakiwa kwenye mwendo, ambapo yatakayokuwa na uzito sahihi yataruhusiwa kuendelea na safari, na yatakayobainika kuzidisha uzito yatazuiwa kwa hatua na taratibu stahiki za kisheria.
"Hii mizani siyo tu itapunguza msongamano wa magari kwenye mizani, bali pia muda unaotumika kupima magari kwenye mizani," aliongeza Meneja huyo wa TANROADS Mkoa wa Mara.
Mhandisi Maribe alisema tayari Serikali imekamilisha malipo ya shilingi milioni zaidi ya 400 ya fidia kwa watu 28 waliokuwa wanamiliki mashamba katika eneo la mradi huo.
"Tumeshalipa fedha zaidi ya shilingi milioni 400 kwa wakulima wa mashamba na wamiliki wa ardhi katika eneo hili la Rubana linalotumika kwa ajili ya ujenzi wa mzani wa kupima magari, kwa hiyo hakuna changamoto ya madai, tunafanya kazi kwa uhuru kuhakikisha tunatimiza adhima ya Serikali,” alisema.
Kwa upande wake Naibu Waziri Kasekenya alisema ziara yake ya kutembelea na kukagua ujenzi wa mizani hiyo imetokana na msukumo wa wabunge wa mkoani Mara.
“Tunahitaji mizani hii ikamilike ili kulindaa barabara zetu, nadhani hii ni mizani bora na ya kisasa Kanda ya Ziwa, na ni muhimu kwenye hii barabara inayounganisha nchi na nchi [Tanzania na Kenya].
“Pamoja na kupima magari yakiwa kwenye mwendo, Serikali pia itafunga 'scanner ' maalumu kwenye mizani hii itakayokuwa na uwezo wa kuona mizigo iliyomo ndani ya makontena.
“Tuendelee kumshukuru Rais wa Awamu ya Sita, Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye mizani hii ukisikia bilioni 22, mkandarasi ana asilimia zaidi ya 50 hakuna anachodai - maana yake Rais anataka barabara anazozijenga ziendelee kudumu na ndio maana anajenga mizani hii kubwa ili kuondoa usumbufu, scanner itakayofungwa itasaidia kudhibiti mtu kupitisha mali ambayo haifahamiki,” alisema Naibu Waziri huyo.
Aidha aliwataka mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha anaukamilisha kwa wakati na ubora stahiki kwa mujibu wa mkataba, huku akiahidi kuwa Serikali itahakikisha malipo yote yanafanyika kwa wakati ili kuondoa visingizio vya ucheleweshaji.
"Tunahitaji kuondoa msongamano wa magari katika mizani lakini tayari tumeshalipa kila kitu hapa, tunahitaji kazi ikamilike kama ilivyopangwa maana hakuna changamoto yoyote, kazi ifanyike kama ilivyosanifiwa,” alisisitiza Kasekenya.
Awali, Meneja wa mradi huo wa ujenzi wa mizani, George Mwandinga alimhakikishia Naibu Waziri Kasekenya kuwa utakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyosanifiwa.
“Kazi zilizobaki ni za muda mfupi lakini za gharama kubwa. Mfano gharama ya mizini pekee ni asilimia zaidi ya 35 [ya gharama zote za utekelezaji wa mradi huo],” alisema Mwandinga.
Hata hivyo alitaja mvua zinazonyesha kuwa kikwazo cha ujenzi huo kwani wakati mwingine wanalazimika kusitisha kazi kwa muda.
Alitaja kikwazo kingine kuwa ni baadhi ya wananchi kukatalia meneo ya kuchimba kifusi kwa sababu za malipo. “Wananchi wanakataa kuchukua hela ili tuchimbe kifusi wakidai hazitoshi, hiyo nayo inachangia kuchelewesha ujenzi,” alisema.
Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri Kasekenya alisema hatua zimeanza kuchukuliwa ikiwemo kuelimisha wananchi hao umuhimu wa barabara.
“Barabara ni za wananchi siyo za serikali, lazima tutumie mawe na kifusi kutoka kwenye maeneo ya wananchi. Hivyo wananchi wanaokatalia vitu hivi wanachelewesha ujenzi.
“Hatuchukui bure, lakini pia hata wewe [mwananchi] unakuwa umesaidia [kufanikisha ujenzi]. Maeneo mengine watu wanaachia bure. Hivyo niombe wananchi pale ambapo Serikali inaomba kwa makubaliano msigeuke.
“Tumeongea na viongozi wa vijiji husika wawashawishi wananchi wao waone umuhimu kwamba barabara hii ni ya kwetu sote.
“Kwa hiyo rai yangu kwa wananchi ni kwmba watambue mizani hii ni kwa ajili ya kusaidia barabara zetu zidumu zaidi, inasaidi mtu asizidishe uzito maana ukizidisha unaharibu barabara,” alisema Naibu Waziri huyo wa Ujenzi na Uchukuzi.
Kwa upande mwingine Naibu Waziri Kasekenya alipata fursa ya kukagua miradi mingine kadhaa ya barabara inayosimamiwa na TANROADS katika wilaya za Tarime, Serengeti na Rorya mkoani Mara.
Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa barabara ya Nyamwigura - Nyamongo (km 25) katika wilaya ya Tarime inayojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 34 ambazo pia zimetolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia.
Chanzo: SAUTI YA MARA
No comments:
Post a Comment