NEWS

Sunday 5 March 2023

TPO yagawa na kupanda miti ikihamasisha uzalendo kwenye taasisi za umma TarimeNa Christopher Gamaina
------------------------------------

TAASISI ya Kizalendo Tanzania (TPO) Wilaya ya Tarime, imegawa na kushiriki kupanda miti zaidi ya 1,700 katika Kituo cha Afya Sirari, Shule ya Msingi Kitagasembe na Shule za Sekondari Bukira na Korotambe - kuhamasisha uzalendo na utunzaji wa mazingira.

Kituo cha Afya Sirari kimepta mgawo wa miti 206, Shule ya Sekondari Bukira (402), Shule ya Msingi Kitagasembe (zaidi ya 500) na Shule ya Sekondari Korotambe (650), yote ikiwa ya mbao na kivuli.

Katika Shule ya Sekondari Bukira

TPO Tarime ilijitolea kufanya shughuli hizo wiki iliyopita, ikiongozwa na Mlezi wake, Joseph Nyabaturi akisaidiana na Mwenyekiti wa Wilaya wa taasisi hiyo, Philipo Lusotola na Mhifadhi Misitu wa Wilaya kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Charles Massawe.

Nyabaturi alitumia nafasi hiyo pia kufundisha wanafunzi wa shule hizo namna nzuri ya kupanda na kutunza miti kwa upendo, ili kudumisha uhifadhi wa mazingira yanayoizunguka jamii.

“Binafsi napenda sana mazingira. Kupanda miti ni utamaduni wa kizalendo na utunzaji wa mazingira,” alisema mlezi huyo wa TPO Tarime na kutoa wito wa kuhamasisha watu kujitolea kufanya vitu vinavyosaidia jamii na kutunza mazingira.

Mlezi wa TPO Wilaya ya Tarime, Joseph Nyabaturi akieleza wanafunzi wa Shule ya Msingi Kitagasembe umuhimu wa kupanda miti na kutunza mazingira.

Lusotola alisema lengo la shughuli hizo ni kuendelea kuhamasisha na kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akisisitiza juu ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira.

Aliongeza kuwa shughuli hizo zinafanyika sambamba na kueneza elimu ya uzalendo kwa wanafunzi ili baadaye wasaidie nchi kuendeshwa katika hali ya utulivu, amani, umoja na upendo.

Mwenyekiti wa TPO Wilaya ya Tarime, Philipo Lusotola (katikati) akihamasisha uzalendo kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Korotambe.

“Kwa hiyo tunajaribu kupandikiza mbegu hii ya kizalendo kwa wanafunzi ili watakapokuwa waweze kusambaza amani na uzalendo katika nchi yetu,” Lusotola alisisitiza.

Mhifadhi Misitu, Massawe, aliishukuru na kuipongeza TPO kwa kujitolea kuunga mkono shughuli za upandaji miti na kuhamasisha utunzaji wa mazingira ya taasisi za umma.

“Viongozi wa TPO Wilaya ya Tarime walikuja kuomba miti tukawapa miti takriban 1,760. Tunawapongeza na niwatie moyo waendelee pia kufundisha wanafunzi kupanda miti na kutunza mazingira kwa sababu ni jambo la kizalendo na linalonufaisha jamii nzima,” alisema Massawe.

Katibu Msaidizi wa TPO Wilaya ya Tarime, Prisca Marwa akipanda mti

Mkuu wa Shule ya Sekondari Bukira, Mwalimu David Jeremiah, Kaimu Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya Sirari, Edicia Modest, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kitagasembe, Hamis Mwita na Mkuu wa Shule ya Sekondari Korotambe, Mwalimu Stephano Wambura waliishukuru na kuipongeza TPO Wilaya ya Tarime kwa juhudi hizo za kizalendo.

“Miti hii itapendezesha mazingira ya shule. Tutaendelea kuipanda na kuhakikisha inakua vizuri. Ninawashukuru wana-TPO pia kwa kutuelekeza namna nzuri ya kuipanda na kuitengeneza kwa upendo ili ikue vizuri, na wamesababisha wanafunzi kujua kwamba kumbe unapopanda miti ni kama unaivisha ardhi nguo nzuri,” alisema Mwalimu Wambura.

Naye mwanafunzi Levina Michael wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Bukira alisema “Nimefurahi sana, ninaishukuru taasisi ya TPO na nitashiriki kutunza miti hii na mazingira ya shule yetu.”

Viongozi wa TPO, Mhifadhi Misitu, Walimu na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Korotambe katika picha ya pamoja shuleni hapo.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages