NEWS

Tuesday 21 March 2023

WWF wazindua Mradi wa Uhifadhi Endelevu wa Dakio la Mto Mara



Na Mara Online News
--------------------------------

SHIRIKA la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF) Tanzania limezindua mradi wa miaka mitatu wa Uhifadhi Endelevu wa Dakio la mto Mara kwa ajili ya kusaidia kuongeza mtiririko wa maji na kuboresha maisha ya wananchi katika bonde la mto huo.

“Mradi huu unafadhiliwa na watu wa Marekani kupitia Shirika lake la Maendeleo la Kimataifa (USAID) na kutekelezwa na Shirika la WWF kwa kushirikia na wadau mbalimbali - hasa Serikali katika wilaya sita (Serengeti, Butiama, Tarime, Rorya, Musoma na Bunda) za mkoa wa Mara,” Mratibu wa mradi huo, Mhandisi Christian Chonya amesema katika hafla ya uzinduzi huo mjini Tarime leo.

Mhandisi Chonya amesema mradi huu utasaidia kutatua changamoto za usalama wa maji na kustahimili mabadiliko ya tabianchi yaliyopo na yanayoongezeka miongoni mwa jamii.

“Mradi huu unatarajia kufikia watu 27,200 kupitia uhifadhi wa rasilimali za maji na mifumo bora ya usambazaji maji,” amebainisha.

Amesema Serikali ya Marekani kupitia Shirika la USAID wanafadhili mradi huo kwa thamani ya Dola za Kimarekani milioni mbili (sawa na Shilingi za Kitanzania bilioni 4.6 kwa miaka mitatu [kuanzia Aprili 2022 hadi Aprili 2025].

Melengo ya mradi huo kwa mujibu wa Mhandisi Chonya, ni kuwezesha taasisi za maji katika uhifadhi wa dakio la mto Mara kushiriki, kuratibu na kutekeleza usimamizi wa rasilimali za maji kwa ushirikiano wa nchi za Tanzania na Kenya zinazochangia mto huo.

Mhandisi Chonya akiwasilisha mada

“Pia kuboresha Maisha ya jamii na kuwezesha usambazaji wa maji kupitia uhifadhi wa rasilimali za maji, kuratibu mapendekezo ya mifumo bora wa malipo ili kuboresha uhifadhi wa vyanzo vya maji kwa ajili ya uhakika wa upatikanaji maji na uhifadhi endelevu wa dakio la Mara,” ameongeza.

Meneja wa Uhifadhi wa Shirika la WWF Tanzania, Lawrence Mbwambo amesema utekelezaji wa mradi huo utasaidia kuboresha maisha ya watu, kuongeza tija katika kilimo na kuwawezesha kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa Mbwabo, mito mingi katika bonde la mto Mara inakabiliwa na upungufu wa maji kutokana na vipindi virefu vya kiangazi, hivyo mradi huo utasaidia pia kuhifadhi misitu na milima iliyopo ili kuvuta mvua itakayochangia kuongeza kiwango cha maji katika mto huo kwa manufaa ya jamii.

Akizungumza kabla ya kukata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele amelishukuru Shirikia la USAID kutokana na ufadhili wa mradi huo, na kutoa wito kwa wadau na wananchi wa maeneo husika kuwapa ushirikiano wa dhati watekelezji wa mradi huo, yaani Shirika WWF ili liweze kufikia malengo yanayokusudiwa.

Kanali Mntenjele akizungumza katika halfa ya uzinduzi huo

Awali, Mwakilishi wa WWF kutoka Marekani, Anis Ragland amesema shirika hilo linaona fahari kusaidiana na Serikali ya Tanzania katika kukabili changamoto za mazingira.

Naye Msimamizi wa USAID Tanzania, Mhandisi Boniphace Marwa amesema matarajio yake ni kuona matokeo ya utekelezaji wa Mradi wa Uhifadhi Endelevu wa Dakio la Mto Mara yanaonekana kwa kuboreka kwa maisha ya wananchi wanaoishi maeneo ya mradi huo, ikiwemo kuwawezesha kupata huduma ya majisafi na salama.

Kwa upande mwingine, Mhandisi Marwa amesisitiza umuhimu wa nchi za Tanzania na Kenya kuendelea kushikiana na sekta binafsi katika utunzaji wa mto Mara na maliasili nyingine zinazouzunguka kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages