NEWS

Wednesday 5 April 2023

Right to Play, AICT Mara wasisitiza elimu kwa watoto wa kike bila kuwakatiliNa Mara Online News
-----------------------------------

SHIRIKA la Right to Play kwa kushirikiana na Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe limeendelea kutumia matamasha ya michezo kwa wanafunzi kuhamasisha elimu kwa watoto wa kike na kukemea vitendo vya ukatili dhidi yao.

Akizungumza wakati wa tamasha la michezo kwa wanafunzi lililofanyika Shule ya Msingi Gwitare iliyopo kata ya Nyamwaga katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) mkoani Mara hivi karibuni, Afisa Mradi kutoka AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Rebeca Bugota alisema watoto wa kike wana haki ya kupewa elimu bora na kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili ili waweze kufikia ndoto zao.

“Hapa kwetu Tarime na Tanzania kiujumla kumekuwepo na mila za kikatili kwa watoto wa kike kama vile ukeketaji, kuachishwa masomo na kuozeshwa katika umri mdogo - jambo ambalo ni hatari kwa watoto hao na linawazuia kutimiza malengo yao.

“Mfano hapa Gwitare kuna mtoto alikeketwa na hivi sasa hata shule ameachishwa, maana yake wanapanga kumuozesha, ndugu zangu huu ni ukatili na haukubaliki,” Rebeca alisisitiza.

Rebeca akizungumza katika tamash hilo

Aidha, Rebeca aliwahimiza wazazi na walezi kujenga utamaduni wa kuwazuia watoto wa kike kwenda maeneo hatarishi, badala yake wawape nafasi ya kusoma na kutambua haki zao.

“Wazazi tutimize wajibu wetu kwa kuhakikisha watoto wote wa kike na kiume wanapata haki sawa ndani ya familia. Watoto wa kike wakisoma watasaidia familia zao kutoka kwenye umaskini,” alisema Afisa Mradi huyo kutoka AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe.

Rebeca alibainisha kuwa Shirika la Right to Play kwa kushirikiana na AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe pia limekuwa likitoa misaada ya vifaa vya elimu kwa wanafunzi wenye uhitaji, wakiwemo watoto wa kike na wale wenye ulemavu.

“Shirika letu limekuwa likitoa mahitaji ya shule kwa watoto wa kike na wale wenye ulemavu wanaopungukiwa mahitaji ili kuwasaidia kutimiza malengo yao ya kielimu na kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili,” alisema.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Gwitare, John Bhoke alilipongeza Shirika la Right to Play kwa kuandaa tamasha hilo la michezo lililobebwa na kaulimbiu inayosema “Ukatili kwa wasichana ni kikwazo kwa maendeleo, tuwalinde na kuwapa fursa sawa”.


“Kupitia tamasha hili najua ujumbe umeeleweka vizuri kwa wanafunzi na wazazi waliohudhuria hapa, hivyo wakatusaidie kuwalinda na kuwaepusha watoto wa kike na mila za kikatili,” alisema Mwalimu John.

Kwa upande wao, wanafunzi wa darasa la saba katika shule hiyo, Mussa Chacha na Happiness Wambura waliahidi kuwa mabalozi wazuri wa kuhmsisha usawa wa elimu kwa watoto wa kike na kiume, sambamba na kupiga vita vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto wa kike, ukiwemo ukeketaji.

“Watoto wa kike waachwe wasome maana wakisoma watakuwa na faida kwa jamii siku zijazo,” alisema Happiness.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages