NEWS

Sunday 30 April 2023

Uwekaji vigingi mpaka wa Hifadhi ya Serengeti wakamilika, RC Mzee sasa ataka maendeleo kwa wananchi Tarime Vijijini



Na Mara Online News
--------------------------------

MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo ametangaza kukamilika rasmi kwa kazi ya uwekaji wa vigingi vya mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na vijiji vinavyopakana nayo katika kata za Nyanungu, Gorong’a na Kwihancha wilayani Tarime.

“Zoezi la kuweka mpaka kati ya kata tatu zinazopakana na mbuga ya Serengeti leo limekamilika rasmi. Naamini kukamilika kwa hili zoezi kutaleta faraja kati ya wananchi, SENAPA (Hifadhi ya Taifa ya Serengeti) na wawekezaji. Sasa naamini hawa watu wote watashirikiana,” amesema RC Mzee na kuongeza kuwa ushirikiano baina ya pande hizo utaharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wanavijiji husika.

“Faraja yangu ni kwamba tutafanikiwa kuwaletea wananchi wetu maendeleo ambayo ndiyo dhamana yetu kubwa,” amesema kiongozi huyo na kutumia nafasi hiyo pia kuwashukuru Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa, Katibu wa chama hicho wa mkoa huo, Lengael Akyoo na wote waliochangia kufanikisha uwekaji vigingi hivyo.

Naye Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Izumbe Msindai amemshukuru Mkuu huyo wa mkoa wa Mara, akisema alisimama imara kuhakikisha uwekaji wa vigingi hivyo unakamilika kama ilivyokusudiwa.

“Kikubwa zaidi ni kwamba zoezi limekuwa ni shirikishi, Serikali imeshiriki, Chama Mkoa kimeshiriki, lakini wananchi kuanzia ngazi ya vijiji wameshiriki na viongozi wao pia wameshiriki, kwa hiyo tunatoa pongezi sana kwa wote walioshiriki kukamilisha zoezi hili,” amesema Msindai.

Aidha, Msindai ameahidi kuwa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) litafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na jamii inayozunguka Hifadhi ya Serengeti.

“Tuna kitengo chetu cha ujirani mwema ambacho kinatekeleza miradi mbalimbali kwa jamii yote inayotuzunguka, na vijiji vya wilaya ya Tarime ni wanufaika… na hadi sasa tunaendelea na miradi mitatu ya elimu na afya katika kata za Nyanungu na Kwihancha.

“Mwakani tumejipanga vizuri, tutachimba mabwawa mwili, lakini tutakarabati mabwawa mawili makubwa yaliyopo. Tumetenga milioni 761 (shilingi) kwa kazi hizo, lakini pia tumeanza kuwashirikisha wananchi ili waweze kunufaika na uwepo wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

“Tumeshaorodhesha wananchi 400 ambao tutawatumia katika shughuli mbalimbali kwa miradi inayotekelezwa ndani ya hifadhi na hii inaanza sasa hivi, haitasubiri mwakani,” amesema Msindai.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Simion Kiles amesema “Tunachohitaji ni kumaliza migogoro iliyokuwepo, watu waheshimu mipaka, TANAPA sasa wachimbie wananchi mabwawa na visima - vitasaidia, nashukuru kwa hili zoezi kuisha salama.”

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages