NEWS

Wednesday 19 April 2023

Wananchi mkoani Mara wamlilia Nimrod Mkono


Nimrod Mkono enzi za uhai wake

Na Mara Online News
---------------------------------

WANANCHI wa mkoani Mara wameeleza kushtushwa na kifo cha wakili na mwanasiasa maarufu Tanzania, Nimrod Mkono aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Butiama kupitia chama tawala - CCM kwa miongo kadhaa.

Taarifa zinasema Mkono amekutwa na mauti wakati akiendelea kupata matibabu nchini Marekani.

Wana-Mara wamesema Mkono alikuwa mbunge wa mfano, mwenye maono na aliyetoa mchango mkubwa wa maendeleo ya kisekta, wakitaja elimu kama moja ya sekta alizozipa kipaumbele wakati wa uongozi wake.

“Hatujawahi kupata mbunge wa mkoani Mara kama huyo mzee, apumzike kwa amani,” mmoja wa wananchi hao aliandika kwenye mitandao ya kijamii jana jioni.

Mkono amekuwa nje ya Tanzania kwa miaka minne tangu 2018, akiripotiwa kuwa kwenye matibabu ya tatizo la kupoteza kumbukumbu (Alzheimer), kulingana na mdogo wake, Zadock Mkono.

Zadock aliviambia vyombo vya habari kwamba kifo cha kaka yake kilitokea jana asubuhi huko Florida, Marekani.

Pamoja na mambo mengine, Mkono atakumbukwa kwa kutumia mamilioni ya fedha zake kugharimia ujenzi wa shule za kisasa katika jimbo la Butiama, ikiwemo Sekondari ya Oswald Mang’ombe ambayo sasa inabadilishwa kuwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia.

#Tunakuhabarisha Uweli na Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages