NEWS

Tuesday, 18 April 2023

Musoma: Mkandarasi aikabidhi NHC jengo la biashara la kisasa lenye thamani ya shilingi bilioni tatu



Na Mwandishi Wetu, Musoma
--------------------------------------------------

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limekabidhiwa rasmi jengo la kisasa la biashara mjini Musoma kutoka kwa Kampuni ya KIULA Engineering Ltd iliyolijenga.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo mjini Musoma jana, Meneja wa kampuni hiyo, Juma Mkwawa alisema mkataba wa ujenzi wa jengo hilo ulikuwa wa miaka miwili ukiwemo mmoja wa uangalizi. “Tumekamilisha ujenzi huu ndani ya muda wa mkataba,” alisema.

Meneja wa mradi wa jengo hilo, Mhandisi Mbuga Mtamwe alisema ujenzi wa jengo hilo lenye ghorofa tano limegharimu takriban shilingi bilioni tatu.

“Tunakabidhi jengo hili kwa ajili ya kuanza matumizi ya upangishaji wa kibiashra, lina lifti mbili za kisasa na limepata vibali vyote vya ukaguzi na matumizi, ikiwemo kutoka makao makuu na OSHA (Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi),” alisema Mhandisi Mtamwe.

Aliongeza kuwa jengo hilo lina maeneo ya ofisi na kumbi za kisasa kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo mikutano na harusi.

Kwa upande wake, Joseph John kutoka NHC Mkoa wa Mara aliishukuru Kampuni ya KIULA Engineering Ltd kukamilisha ujenzi wa jengo hilo kwa wakati, akisema pamoja na faida nyingine limeongeza mali za shirika hilo na kupendezesha mji wa Musoma.

“Tunashukuru kwa sababu jengo hili limeongeza thamani ya mali za Shirika la Nyumba la Taifa katika mkoa huu wa Mara, limependezesha mkoa wetu, na kwa ujumla ndilo jengo ambalo ni zuri kuliko yote hapa mjini, hivyo tunawakaribisha wafanyabiashara kuchangamkia fursa hii,” alisema John.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages