NEWS

Monday 26 June 2023

Chandi achangisha milioni 15 harambee ya Kanisa Katoliki Serengeti
Na Mwandishi wa
Mara Online News
--------------------------

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa amefanikiwa kuchangisha shilingi milioni 15 katika harambee ya Kanisa Katoliki la Mtakatifu Francisco wa Asizi lililopo mjini Mugumu, wilayani Serengeti.

Harambee hiyo ilifanyika kanisani hapo jana, kwa lengo la kuchangia ununuzi wa vifaa vya kisasa vya Kwaya ya Mama Maria Mtakatifu Mama wa Mungu, ili kuiwezesha kupanua shughuli za uinjilisti.


Katika harambee hiyo, Chandi ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi, alisindikizwa na rafiki zake mbalimbali, wakiwemo wafanyabiashara na makada wenzake wa chama tawala - CCM hadi kufanikisha upatikanaji wa kiasi hicho cha shilingi milioni 15.

Chandi ambaye pia ni muumini wa Kanisa Katoliki, alitumia nafasi hiyo pia kuwahamasisha waumini wenzake kuendelea kumtegemea na kumtumainia Mwenyezi Mungu, kwani ndiye muweza wa yote na hakuna jambo linaloshindikana mbele yake.

“Tuendelee kumtii Mwenyezi Mungu kwa kufanya yale yote yaliyo mema. Waumini wenzangu kumbukeni milango inafunguka pale ambapo kuna changamoto,” alisisitiza.
Chandi (kulia) akipokea zawadi ya kikombe kutoka kwa mwanakwaya wakati wa harambee hiyo

Kwa upande wake, mgeni maalam katika harambee hiyo, Simion Lyimo Nyansaho ambaye ni Mkurugenzi wa Masoko wa Benki ya Azania Tanzania, alishukuru kwa kupata nafasi ya kujumuika katika tukio hilo la kiroho.

“Katika maisha yangu navipa kipaumbele vitu vitatu; ambavyo ni kumtanguliza Mungu (huduma ya Mungu), kipaumbele cha pili ni afya maana bila afya njema huwezi kufanya chochote katika maisha, na cha tatu ni elimu ambayo ni ufunguo wa maisha, ndio maana nashiriki kikamiilifu mnaponihitaji.

“Hivyo narudia kusema asanteni sana kwa kujumuika na ninyi kwa siku ya leo na kufanikisha malengo yenu ili kuimarisha uinjilishaji,” alisema Mkurugenzi Nyansaho.

Mkurugenzi Nyansaho akizungumza katika harambee hiyo

Naye Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Francisco wa Asizi ya mjini Mugumu, Padre Joel aliwashukuru waumini, mgeni rasmi na waalikwa wote kwa kufanikisha harambee hiyo ambayo alisema imetimiza lengo, huku akiwahimiza watu wote kumtumainia Mwenyezi Mungu asiyeshindwa na chochote.

Paroko Joel akizungumza katika harambee hiyo#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages