NEWS

Monday 26 June 2023

Professor Mwera yawatangazia ofa wanafunzi sekondari za kutwa za serikali

Mkurugenzi wa PMF, Hezbon Peter Mwera.


Na Mwandishi wa
Mara Online News
-----------------------------

TAASISI ya Professor Mwera (PMF) ametangaza nafasi kwa wanafunzi shule za sekondari za kutwa za serikali - wanaohitaji kusoma wakiwa wanaishi bweni katika Shule ya Sekondari ya Tarime Mchanganyiko kuanzia sasa, kisha kurudi kwenye shule zao kufanya Mtihani wa Taifa ya Kuhitimu Kidato cha Nne.

“Tunatoa nafasi hizo ambapo mwanafunzi atalipa ada ya shilingi milioni moja kwa mwaka kwa ajili ya chakula, malazi (bweni), kusoma, kufanya mitihani na majaribio ya kutosha, lakini mwisho wa siku warudi kwenda kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne kwenye shule zao.

“Hivyo wanafunzi watakaojitokeza kuhamia Sekondari ya Tarime Mchanganyiko kuanzia Julai mwaka huu watalipa ada ya nusu mwaka ambayo ni shilingi 500,000,” amefafanua Hezbon Peter Mwera, Mkurugenzi wa Taasisi ya Professor Mwera inayomiliki shule hiyo.

“Tumeamua kutoa nafasi hizi ili kusaidia watoto wetu maana unajua wanafunzi wakikaa bweni wanapata muda wa kutosha kusoma hadi usiku tofauti na ilivyo katika shule za kutwa,” amesema Hezbon katika mazungumzo na Mara Online News ofisini kwake leo.

Ameongeza kuwa fursa hiyo pia itawaepushia wanafunzi husika changamoto za kwenda shule na kurudi nyumbani kila siku, lakini pia itazipunguzia shule za sekondari za kutwa za serikali msongamano wa wanafunzi.

Mkurugenzi Hezbon amesema wanafunzi watakaochangamkia fursa hiyo watapewa ofa ya kusoma bure mojawapo ya fani/ kozi za ufundi zinazotolewa katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime kinachomilikiwa pia na Taasisi ya Professor Mwera.

Hezbon ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Kanda ya Ziwa, ametaja fani za ufundi zinazotolewa chuoni hapo kuwa ni za umeme, magari, kompyuta, ushonaji/chereheni, udereva, bomba, secretarial, maabara, utalii na hoteli, muziki, video production na ICT.

Shule ya Sekondari ya Tarime mchanganyiko na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime vipo katika kata ya Turwa, umbali wa kilomita mbili kutoka katikati ya mji wa Tarime mkoani Mara.

Wakati huo huo, wanafunzi wote 21 waliohitimu na kufaulu Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari ya Tarime Mchanganyiko mwaka 2022, wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo mbalimbali mwaka huu.

Kati ya hao, wanafunzi 17 wamechaguliwa kwenda kidato cha tano kwenye shule za sekondari za bweni na wanne kwenda vyuo vya kati katika mikoa mbalimbali nchini.

“Tunawakaribisha wanafunzi wanaotaka kujiunga na hii shule yetu, tuna nafasi za kidato cha kwanza hadi cha nne, ada kwa mwanafunzi wa bweni ni shilingi milioni 1.5 na wa kutwa ni shilingi milioni moja kwa mwaka. Kwa maelezo zaidi tupigie simu kupitia namba 0768901641 au 0784471576,” amesema Hezbon.


#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages