Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda (kulia) akipokea nakala ya Sauti ya Mara kutoka kwa Mhariri Mtendaji wa gazeti hilo, Jacob Mugini.
Na Mwandishi wa
Mara Online News
----------------------------
MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Said Mohamed Mtanda, ameahidi kulipatia Gazeti la Sauti ya Mara ushirikiano wa dhati katika kutangaza fursa za maendeleo ya kiuchumi na kijamii zilizopo ndani ya mkoa huo uliojaaliwa kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili muhimu kama vile madini, Hifadhi ya Taifa Serengeti, Ziwa Victoria na ardhi inayostawisha mazao mbalimbali ikiwemo kahawa aina ya Arabica inayotamba kwenye soko la dunia.
RC Mtanda ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo maalumu na wahariri wa gazeti hilo, Jacob Mugini na Christopher Gamaina mjini Tarime, mapema leo Juni 21, 2023.
Amempongeza Mugini ambaye pia ni Mkurugenzi wa gazeti hilo, akisema anastahili kuungwa mkono na Serikali ili ubunifu aliouonesha usaidie kuchochea maendeleo ya kisekta katika mkoa wa Mara na Taifa kwa ujumla.
“Sauti ya Mara nawaona mnafanya vizuri na mnaunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali kwa maendeleo ya wananchi, na sisi tunawaahidi ushirikiano,” amesema kiongozi huyo wa mkoa katika kikao hicho ambacho pia kimewashirikisha baadhi ya viongozi wakiwemo Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Daniel Komote.
Hivyo RC Mtanda ametaka viongozi wa wilaya na halmashauri za mkoa huo kukipa ushirikiano chombo hicho cha habari kiendelee kutekeleza majukumu yake kwa manufaa ya umma. Gazeti la Sauti ya Mara lina vyombo dada vya habari ambavyo ni Mara Online News na Lake Zone Watch kinachoripoti habari na makala kwa lugha ya Kiingereza.
Vyombo vyote hivyo vimejikita katika kuripoti habari na makala za maendeleo ya jamii, huku kipaumbele kikiwa kwenye sekta za uhifadhi, utalii, maji, madini, uvuvi, elimu, afya, kilimo na miundombinu ya barabara.
RC Mtanda anaendelea na ziara yake ya kikazi katika wilaya za mkoa wa Mara, ambapo ratiba yake leo ni kuhutubia vikao vya mabaraza ya madiwani wa halmashauri za Tarime Mji na Vijijini.
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment