NEWS

Friday 16 June 2023

RC Mtanda anasua malori 30 mikononi mwa TRA, ayaonya kutotorosha chakula kwenda nje ya nchi


Na Mwandishi wa
Mara Online News
------------------------------

MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Said Mohamed Mtanda ameagiza kuachiwa kwa malori zaidi ya 30 yenye shehena ya nafaka za chakula - yaliyokuwa yameshikiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa siku kadhaa katika kituo cha Kirumi wilayani Rorya, lakini kwa sharti la kutotorosha chakula hicho kwenda nje ya nchi.

Hayo yamejiri leo Ijumaa asubuhi, baada ya RC Mtanda kutembelea eneo hilo na kuwaomba radhi wafanyabiashara wenye malori hayo, akisema kilichotokea ni kinyume na maagizo ya serikali.

“Kwanza niwaombeni radhi kwa sababu kilichotokea sicho ambacho serikali iliagiza. Mwananchi yeyote ambaye ana nyaraka ya kusafirisha chakula nje ya nchi anaruhusiwa kusafirisha, isipokuwa serikali ikitoa waraka wa kukataza tena kwamba kuanzia leo kibali hiki kimefutwa - maana yake vibali hivyo hata kama unavyo vinakuwa vime- expire (vimeisha muda wake).

“Kwa hiyo hapa walikuwa na haki ya kukusimamisha usiendelee na safari yako, sasa ninyi mmenihakikishia kwamba ni wafanyabiashara wa Tanzania, mnapeleka nafaka zenu Tarime, kwa hiyo maelekezo yetu ni kwamba tutawaruhusu kuelekea Tarime lakini katika masharti kwamba tutawasindikiza mpaka Tarime ili kila mtu atueleze chakula chake anakipeleka kwenye ghala gani, kwa sababu muongozo unasema lazima tusajili maghala.

“Tunafanya hivi ili kudhibiti utoroshwaji wa chakula chetu kwenda nje ya nchi. Sisi tuko mpakani na kuna biashara nyingi ya magendo inafanyika, na serikali tumeamua kudhibiti utoroshwaji wa chakula kwenda nje ya nchi.

“Lakini pia ninawaonya msije mkafikiri mna ujanja sana, kwamba mnaweka chakula kwenye yale maghala halafu usiku mnatorosha kwenda mpakani, mtafilisika na nafaka zenu zitakamatwa, na utakapokamatwa maana yake wewe ulikuwa unafanya biashara ya magendo, sasa msipoteze muda wenu serikali iko macho… chakula hakitasafiri kwenda nje ya nchi bila kufuata utaratibu,” amesisitiza RC Mtanda.

Katika ziara hiyo RC Mtanda ameongozana na Wakuu wa Wilaya; Juma Chikoka wa Rorya na Kanali Michael Mntenjele wa Tarime, miongoni mwa wajumbe wengine wa kamati za ulinzi na usalama za wilaya hizo na mkoa wa Mara.


#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages