Na Mwandishi wa
Mara Online News
------------------------------
KANISA la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Right to Play wametumia maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika 2023, kuhamasisha wazazi na jamii nzima kuwapa watoto wote elimu bora na iliyo jumuishi, sambamba na kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku hiyo yaliyofanyika katika kata ya Itiryo wilayani Tarime kwa ushirikiano na Halmashauri ya Wilaya hiyo jana, Afisa Mradi kutoka AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Rebeca Bugota alisisitiza kuwa wazazi na watu wote katika jamii wana wajibu wa kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi kwa manufaa ya taifa.
“Tunapoadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika tunaendelea kutoa wito kwa wazazi na jamii kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya kikatili vinavyowaweka kwenye mazingira hatarishi, tuwatengenezee mazingira salama ya kukua na kujifunza kwa sababu tunafahamu ni taifa la kesho ambalo tunalitegemea,” alisema Rebeca.
Alisema mustakabali wa maendeleo ya kisekta ya taifa unategemea uwekezaji mzuri kwa watoto wote - unaohusisha malezi, elimu, ulinzi na usalama wao.
“Kwa hiyo tukitaka tuone matunda mazuri kwa watoto wetu ni lazima tuwekeze kwao, tuwape elimu tuwatunze, tuwalinde na tuwape haki zao zote za msingi,’ alisisitiza Rebeca.
Rebeca Bugota |
Maadhimisho hayo ya Siku ya Mtoto wa Afrika - yaliyobebwa na kaulimbiu inayosema “Zingatia Usalama wa Mtoto katika Ulimwengu wa Kidijitali”, yalipambwa na michezo mbalimbali ya wanafunzi wa shule za msingi na washindi kupewa zawadi.
AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe wanashirikiana na Right to Play katika kulinda, kuelimisha na kujenga uwezo kwa watoto na vijana kupitia michezo ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Washirika hao wanaendesha shughuli zao katika kata za Itiryo, Nyansincha na Nyamwaga ambako wanatekeleza mradi wa kielimu unaolenga kukuza ubora wa elimu na iliyo jumuishi kwa lengo la kuhakikisha watoto wote wanapomaliza shule wawe wanajua kusoma, kuhesabu na kuandika.
“Mambo makubwa tunayofanya ni kujenga uwezo kwa walimu, lakini pia kuhakikisha mtoto anapata elimu bora. Tunafanya matamasha ya michezo, midahalo na tunatoa mafunzo kwa wazazi.
”Lengo kubwa ni kuiwezesha jamii kujua vikwazo vya kielimu vinavyomkabili mtoto na namna ya kuvishughulikia ili mtoto anapokwenda shuleni aweze kujifunza vizuri na kuelewa.
“Tunasaidia watoto wenye mahitaji maalumu, wakiwemo wenye ulemavu na watoto wa kike wenye umri wa kwenda shule tunahakikisha wanaandikishwa na kuwasaidia mahitaji ya shule ili kuhakikisha wanapata fursa ya kusoma,” alisema Rebeca.
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment