Na Mwandishi Wetu, Mara
-------------------------------------
MAKUNDI ya tembo yameendelea kuingia na kusababisha madhara mbalimbali ndani ya vijiji vinavyopakana na maeneo ya uhifadhi katika wilaya za mkoani Mara, licha ya kuwepo juhudi zinazofanywa na wadau wa uhifadhi ili kudhibiti wanyamapori hao.
Kwa mujibu wa viongozi wa kata na vijiji husika, inavyoonekana ni kama juhudi za wadau zimegonga mwamba, kwani tembo wameendelea kuharibu mazao mashambani, kuua watu na mifugo vijijini.
"Tatizo bado lipo, na linaongezeka, mwezi wa nne (Aprili 2023), tumezika mtu aliyeuawa na tembo akiwa kwenye malisho ya mifugo kijijini,” alisema Diwani wa Kata ya Nagusi wilayani Serengeti, Andrea Mapinduzi Amos katika mazungumzo na Sauti ya Mara, wiki iliyopita.
Mapindunzi alisisitiza kuwa tembo wameendelea kutishia maisha ya wananchi na mifugo, sambamba na kufanya uharibifu mkubwa wa mazao ya chakula na biashara katani humo.
"Kipindi hiki cha mavuno wanavijiji, hususan vijana wanalazimika kwenda kufukuza tembo kila siku. Wadau wakiwemo TAWA na Grumeti Reserves wanatupatia misaada ya vifaa kama vile toshi za mwanga mkali na baruti za kulipua lakini hatujaweza kuwadhibiti wanyama hawa, yaani tatizo linazidi kuwa kubwa.
“Tunavyozungumza leo muda mfupi uliopita nimepigiwa simu kwamba tembo wako kijijijini, kwa hiyo natakiwa kuomba msaada wa gari vijana wasaidiane kuwafukuza,” alisema.
Naye Diwani wa Kata ya Kwihancha wilayani Tarime, Ragita Ragita, alisema wananchi katani humo wako katika hatari ya kukumbwa na baa la njaa kutokana na mazao waliyolima kuendelea kupukutishwa na tembo.
“Hata jana tembo walikula mahindi ya wanavijiji. Tembo hawajadhibitiwa kabisa. Mimi kama kiongozi nimeshatoa taarifa za uharibifu unaofanywa na tembo nimechoka. Hawa wanyama wametuletea shida ya njaa, lakini pia wananyima wananchi usingizi,” alisema Ragita.
Aidha, Ragita alizishutumu mamlaka husika kwa kutotekeleza wajibu wa kulipa wananchi fidia na vifuta jasho kutokana na madhara yanayosababishwa na tembo.
“Tulishapeleka maombi ya fidia na vifuta jasho mpaka imefikia hatua tumeona ni kama tunacheza mchezo wa Pwagu na Pwaguzi, yaani mpaka tumeamua kuacha, maana hakuna utekelezaji,” alisema diwani huyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Park Nyigoti wilayani Serengeti, Mtiro Gekora Kitigani alisema ingawa walishaunda kikosi cha kufukuza tembo kwa msaada wa wadau wa uhifadhi, bado kero ya wanyamapori hao haijafutika kijijini kwake.
“Wiki jana [tembo] waliingia wakafukuzwa, lakini wanaweza kurejea tena maana hili tatizo halijaisha, msimu wa mavuno ndio wanakuwa wanashambulia mazao kwa wingi,” alisema Mtiro na kuongeza kuwa mwaka jana mkazi wa kijiji hicho mwenye umri wa miaka 80 aliuawa na tembo akiwa nyumbani kwake usiku.
“Hawa wanyama wakiingia shambani hata kama ni ekari tano wanakula wanamaliza, mkulima anaambulia patupu,” aliongeza mwenyekiti huyo.
Mazao yanayoshambuliwa zaidi na tembo kwa mujibu wa viongozi hao, ni mahindi, mtama, viazi, mpunga, mihogo, alizeti na pamba.
Chanzo: SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment