NEWS

Friday 28 July 2023

Barrick North Mara wajenga zahanati mpya, waikabidhi kwa Serikali ya Kijiji MatongoMwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matongo, Daudi Itembe (katikati) akizungumza wakati wa makabidhiano ya zahanati mpya ya Kenyangi iliyojengwa na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, leo Julai 28, 2023.
-----------------------------------------------------
Na Mwandishi wa

Mara Online News
-------------------------

MGODI wa Dhahabu wa Barrick North Mara umekabidhi zahanati mpya ya kisasa ya Kenyangi - uliyoijenga katika kijiji cha Matongo kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

Meneja Mkuu (GM) wa Mgodi huo, Apolinary Lyambiko amekabidhi jengo la zahanati hiyo, nyumba pacha (two in one) ya watumishi na choo kwa Serikali ya Kijiji hicho leo Julai 28, 2023.Akizungumza wakati wa makabidhiano ya zahanati hiyo, GM Lyambiko amesema uboreshaji wa huduma za afya ni moja ya maeneo manne ambayo Kampuni ya Barrick inayapa kipaumbele katika jamii zinazoishi jirani na migodi yake.

Mbali na afya, ametaja sekta nyingine zinazopewa kipaumbele katika kampuni hiyo ya uchimbaji madini kuwa ni elimu, maji, usalama wa chakula na uchumi.

“Hapa ni mwanzo, tupo pamoja ili kuhakikisha huduma za afya zinaimarika hapa Matongo. Wadau wetu wakubwa ni jamii ambayo inazunguka mgodi na mahusiano bora ni jambo muhimu,” amesema GM Lyamabiko.


GM Lyambiko na viongozi wengine wakikagua jengo la zahanati hiyo

Diwani wa Kata ya Matongo, Godfrey Kegoye ameushukuru mgodi huo kwa kujenga zahanti hiyo, na kuomba ofisi ya Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kuwahisha utaratibu wa kuanza kuwapatia wananchi huduma za afya.

“Tunapenda kutoa shukrani kubwa kwa Mgodi wa Barrick North Mara kwa kutimiza ahadi ya kutuhamishia zahanati [kutoka jirani na mgodi], hata iliyokuwepo haikuwa na ubora mzuri kama hii. Bado tutazidi kushirikiana,” amesema.

Diwani Kegoye (kushoto) akimshukuru GM Lyambiko wakati wa makabidhiano hayo

Kegoye na viongozi wa kijiji cha Matongo wametumia nafasi hiyo pia kummwagia sifa mkandarasi mzawa aliyetekeleza mradi huo - ambaye ni Kampuni ya PKM, wakisema ni mfano wa kuigwa.

“Mkandarasi amefanya kazi nzuri na ni mtu ambaye anajisimamia,” amesema diwani huyo anayetokana na chama tawala - CCM.

Awali, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matongo, Daudi Itembe ameushukuru Mgodi wa Barrick North Mara na mkandarasi huyo kwa kufanikisha ujenzi wa zahanati hiyo ambayo pia imewekewa miundombinu kwa ajili ya kutumiwa na watu wenye ulemavu.

“Cha kwanza sisi kama Serikali ya Kijiji ni kushukuru mgodi, na bahati nzuri zahanati imekamilika, mataminio yetu sasa ni kuona inaanza kuhudumia wananchi wetu,” amesema Itembe.


Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Dkt Joseph Mziba ameushukuru mgodi huo kwa kujenga zahanati hiyo, na kuahidi huduma bora kwa wananchi.

“Nipende kuwashukuru Barrick North Mara kwa kutuwekea zahanati hii hapa, inawezekana kwa baadaye ikapandishwa hadhi kuwa kituo cha afya,” amesema Dkt Mziba na kuongeza kwamba msukumo utakuwa ni kuifanya kuwa moja ya zahanati bora katika halmashauri hiyo.

Naye Msimamizi wa Miradi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Ibrahim Msomi amewakumbusha watumishi wa zahanati hiyo kuzingatia utunzaji wa jengo la makazi yao ili lidumu muda mrefu kwa manufaa ya wengi.

Watumishi wawili wa zahanati hiyo wametambulishwa wakati wa hafla hiyo ya makabidhiano, huku nyumba yao ikionekana kuwa kivutio cha aina yake katika eneo hilo.

Sehemu ya mbele ya nyumba pacha (two in one) ya watumishi wa zahanati mpya ya Kenyangi

Hafla ya makabidhiano ya majengo ya zahanati hiyo ya Kenyangi imehudhuriwa pia na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Idara ya Mahusiano Barrick North Mara, Safarani Msuya na Mkurugenzi wa Kampuni ya PKM, Aron Maisa, miongoni mwa viongozi wengine.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages