NEWS

Tuesday 4 July 2023

Bilioni 1 za fidia, upimaji viwanja zahofiwa ‘kupigwa’ na wajanja’ Rorya 

NA MWANDISHI WETU, Rorya
-------------------------------------------

SHILINGI bilioni moja zilizotolewa mkopo na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kugharimia ulipaji fidia na upimaji viwanja kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya kimkakati wilayani Rorya zinahofiwa ‘kuliwa na wajanja wachache’, Sauti ya Mara inaripoti.

Uchunguzi uliofanywa na Sauti ya Mara kwa siku kadhaa umebaini kuwa fedha hizo ziliombwa na Mbunge wa Rorya, Jafari Chege ili kulipa wananchi fidia waweze kuachia ardhi yenye ukubwa wa ekari 20 kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi katika eneo la Mika.

Ulipaji wa fidia ungefuatiwa na upimaji wa viwanja kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya kibiashara katika eneo hilo, ambapo fidia na upimaji pekee vilitengewa bajeti ya shilingi milioni 184.

Imeelezwa kuwa dhumuni la ujenzi wa stendi hiyo ni kuwezesha mabasi ya kutoka nchi jirani ya Kenya, Sirari na Tarime kuingia kabla ya kuendelea na safari kuelekea miji ya Musoma, Bunda, Mwanza na Dar es Salaam na hata yanaporudi, lengo likiwa kuchochea ukuaji wa uchumi katika wilaya ya Rorya.

Aidha uchunguzi umebaini kuwa shilingi milioni 500 ilikuwa ni bajeti ya kulipa fidia na kupima viwanja kwa ajili ya kujenga ofisi za idara za Uhamiaji na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), lakini pia soko la kimataifa katika eneo la Kilongwe lililopo mpakani na nchi ya Kenya.

Kiasi kinachobaki, yaani shilingi zaidi ya milioni 300 ilikuwa ni bajeti ya kulipa wanarasimishaji wa maeneo ya miji inayokuwa ambayo ni Shirati, Utegi, Mika, Nyanchabakenye na Kinesi.

“Ni kweli mimi ndiye niliomba huo mkopo wa bilioni moja, kama wananchi wangelipwa fidia na viwanja kupimwa katika maeneo hayo kwa ajili ya ujenzi wa miradi hiyo ya kimkakati, wafanyabiashara wangenunua viwanja na tungepata fedha za kulipa huo mkopo, lakini cha kushangaza hakuna kilichofanyika.

“Kimsingi kama kuna ubadhirifu wowote wanaopaswa kuhusika ni pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri na Mkurugenzi,” alisema Mbunge Chege alipoulizwa na Sauti ya Mara kwa njia ya simu juzi.


RC ataka wahusika
wachukuliwe hatua

Akiwa katika ziara ya kiofisi wilayani Rorya hivi karibuni, Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Said Mohamed Mtanda aliziagiza mamlaka husika kufuatilia na kuchukua hatua dhidi ya watumishi watakaothibitika kuhujumu fedha hizo.

Katika agizo lake hilo alitaka aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kabla ya kuhamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti afuatiliwe mpaka ‘kieleweke’.

“Wamechukua bilioni moja wamepima viwanja lakini katika mchakato wote ule ilikuwa ni ‘one man show’, ofisi ya ardhi ndiyo ilikuwa ikiwajibika, na ikumbukwe hawa wataalamu wa ardhi hawako moja kwa moja kinidhamu kwa Mkurugenzi [wa Halmashauri], wako chini ya Kamishna wa Ardhi, kwa hiyo wakati mwingine wanajigeuza kambale hawataki kumsikiliza Mkurugenzi, wanakuwa na kiburi na jeuri.

“Kwa hiyo hela imekuja bilioni moja lakini anayedaiwa ni halmashauri, wanajua wenyewe walichokifanya, hakuna kiwanja na wala hati iliyotoka hadi leo, na amehamishiwa Serengeti.

“Nimeagiza baraza maalumu kule lifanyike, atolewe kule Serengeti na Kamishna wake wa Ardhi aje kwenye baraza waseme kweli, ili tumjue nani ambaye amepoteza mapato ya serikali, nani ambaye ameitia halmashauri hasara na hatutasita kumchukulia hatua kali,” alisisitiza RC Mtanda.

Sauti ya Mara inaendelea na juhudi za kuwapata Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kwa ajili ya kuzungumzia suala hilo. 

Chanzo: SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages