NEWS

Thursday 27 July 2023

Jeshi latangaza mapinduzi dhidi ya Rais Bazoum nchini Niger



WANAJESHI wa Niger katika Afrika Magharibi wametangaza mapinduzi kupitia televisheni ya taifa, wakisema wamevunja katiba, kusimamisha taasisi zote na kufunga mipaka ya nchi hiyo.

Rais wa Niger, Mohamed Bazoum amekuwa akishikiliwa na wanajeshi kutoka kikosi cha walinzi wa rais tangu mapema jana Jumatano.

Aliahidiwa "uungwaji mkono usioyumba" wa Washington kwa simu kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres pia alisema amezungumza na Rais na kumpa uungaji mkono kamili wa Umoja huo.

Bazoum ni mshirika mkuu wa Magharibi katika vita dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu katika Afrika Magharibi.

Nchi mbili jirani; Mali na Burkina Faso, zimekumbwa na mapinduzi yaliyochochewa na maasi ya makundi ya Jihadi katika miaka ya hivi karibuni.

Katika nchi zote hizo mbili, viongozi wapya wa kijeshi wametofautiana na Ufaransa, koloni la zamani, ambalo pia liliwahi kuitawala Niger.

Katika tangazo la televisheni jana Jumatano, Kanali Maj Amadou Abdramane, pamoja na askari wengine tisa waliovalia sare nyuma yake, walisema: "Sisi, vikosi vya ulinzi na usalama... tumeamua kukomesha utawala unaoujua. Hii inafuatia kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama, na utawala mbovu wa kiuchumi na kijamii."

Pia alisema taasisi zote nchini Niger zimesimamishwa kazi na wakuu wa wizara watasimamia shughuli za kila siku.

Jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi, Ecowas imesema "inalaani kwa maneno makali jaribio la kunyakua mamlaka kwa nguvu". BBC

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages