NEWS

Wednesday 19 July 2023

Luhemeja aridhishwa na utekelezaji mradi wa usafi wa mazingira Musoma

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Cyprian Luhemeja (mwenye fulana nyekundu) akiwa katika ukaguzi wa mradi wa Uboreshaji wa Usafi wa Mazingira Musoma jana. Wa pili kulia ni MD wa MUWASA, Mhandisi Nicas Mugisha.

----------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Musoma
---------------------------------------

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Cyprian Luhemeja ameeleza kuridhiswa na maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa Uboreshaji wa Usafi wa Mazingira Musoma ambao unagharimu shilingi bilioni 36. 

 
Hata hivyo Mhandisi Luhemeja amemtaka mkandarasi wa mradi huo ambaye ni Kampuni ya China Civil Engineering Construction Cooperaton (CCECC) kumaliza kazi iliyobaki kwa wakati uliopangwa.

“Mpaka sasa nimeridhidhwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huu, lakini nisisitize kuwa hakutakuwa na muda wa ziada,” Naibu Katibu Mkuu huyo ambaye yupo mkoani Mara kukagua miradi mbalimbali yenye thamani ya mabilioni ya fedha alisema jana.

Alitoa wito wa kuhamasisha wananchi kutunza mradi huo kwa manufaa ya kizazi cha sasa vijavyo.

“Mradi huu wa uboreshaji usafi wa mazingira Musoma unatumia gharama kubwa. Kiasi cha shilingi bilioni 36 zimewekezwa kukamilisha mradi, niwaombe wananchi kuutunza na kuuthamini,” alisema Mhandisi Luhemeja.


Awali, akitoa taarifa ya mradi huo kwa kiongozi huyo, Mkurugenzi Mtendaji (MD) wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA), Mhandisi Nicas Mugisha alisema mradi huo utakuwa suluhisho la uondoaji wa majitaka katika Manispaa ya Musoma.

“Tumekuwa tukiwekeza sana katika huduma ya majisafi na salama. Sasa imebidi tuangalie namna ya kuondosha majitaka na mradi huu ni muarobaini wa tatizo la majitaka mjini Musoma,” Mhandisi Mugisha alisema.

Kwa mujibu wa MD huyo wa MUWASA, mji wa Musoma ambao umezungukwa na Ziwa Victoria haujawahi kuwa na mradi kama huo wa kudhibiti maji taka licha ya kuwa takriban asilimia 80 ya majisafi yakishatumika yanakuwa majitaka.

Kwa upande wake Mhandisi Gift Kimaro kutoka Kampuni ya JKW ambayo ndiyo Mkandarasi Mshauri wa mradi huo, alisema kazi inafanyika usiku na mchana ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages