NEWS

Monday 17 July 2023

Rais Samia aviagiza vyombo vya ulinzi na usalama vijikite zaidi katika kuzuia uhalifu badala ya kukamata na kuhukumu

Rais Samia Suluhu Hassan (kulia) akipokea ripoti ya Tume kutoka kwa Jaji mstaafu, Mohamed Chande Othman, Ikulu jijini Dar es Salaam juzi. (Picha na Ikulu)
---------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
----------------------------------------------

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ametaka kipaumbele cha vyombo vya ulinzi na usalama kiwe kuzuia utendaji wa makosa badala ya kukamata na kuhukumu.

Alitoa agizo hilo Ikulu jijini Dar es Salaam Jumamosi iliyopita, wakati wa kupokea rasmi ripoti ya Tume ya wajumbe 11 aliyoiunda kuangalia jinsi ya kuboresha taasisi za haki jinai nchini.

Sambamba na hilo Rais Samia alivitaka vyombo vya jinai kuwa na mfumo unaosomana katika uendeshaji, ili kurahisisha ufuatiliaji pamoja na kuzuia mfumo wa upelelezi kutoa mwanya wa rushwa.

Alizitaka taasisi za haki jinai kufanya marekebisho ambayo hayana gharama za kifedha katika mifumo yao ya kiutendaji ili kuleta haki kwa wananchi.

Rais Samia pia alielekeza kufanyiwe kazi masuala ya kuheshimu watuhumiwa kwenye ukamataji, upelelezi na uendeshaji wa mashtaka mbalimbali ili haki iweze kutendeka.

Tume hiyo ya Haki Jinai iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman, ilikusanya maoni kutoka taasisi 12 kwa lengo la kupata ushauri na mapendekezo ya namna bora ya kuimarisha mfumo na utendaji kazi wa taasisi zinazohusika na haki jinai.

Awali, akiwasilisha ripoti hiyo kwa Rais Samia, Jaji Chande alisema Tume imebaini kuwepo kwa mnyororo wa udhaifu katika mfumo mzima wa haki jinai.

Alisema udhaifu huo upo katika maeneo yanayo husika na kubaini na kuzuia uhalifu, kukamata na kupeleka watuhumiwa vituo vya polisi, uchunguzi na upelelezi wa makosa ya jinai.

Udhaifu mwingine ambao Tume imeubaini, alisema upo kwenye masuala ya uandikishaji wa mashtaka, usikilizwaji wa kesi za jinai mahakamani na kwa watu waliotiwa hatiani na kutumikia vifungo gerezani.

Pia, Tume hiyo imebanini udhaifu kwenye makosa ya jinai unaonekana hasa katika mfumo mzima wa kubaini wahalifu, kuwakamata na kuwapeleka watuhumiwa vituo vya polisi na gerezani.

Jambo jingine ambalo Tume hiyo imebaini halifanyiki kama inavyotakiwa, ni kuhusiana na masuala ya adhabu mbadala, maisha ya wafungwa wanapomaliza vifungo vyao na pale wanaporejea uraiani.

“Tume imebaini kuwa hakuna mkakati wa kubaini na kuziuia uhalifu, ukosefu huo umesababisha vyombo vya utekelezaji wa sheria, kujikita zaidi kwenye ukamataji badala ya kuzuia uhalifu,” alisema Jaji Chande.

Chanzo: SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages