NEWS

Tuesday 11 July 2023

RC Mtanda akagua ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege Musoma, atoa maelekezo kwa mkandarasi

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda (katikati mbele) akikagua ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege Musoma leo. Kushoto (mbele) ni Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe.
----------------------------------------------------
Na Mwandishi wa
Mara Online News
--------------------------

MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Said Mohamed Mtanda amekagua maendeleo ya mradi wa ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege Musoma, na kutoa maelekezo mbalimbali ili kuharakisha utekelezaji wa mradi huo.

Amefanya ziara hiyo leo Julai 11, 2023, ambapo pamoja na mambo mengine, amehimiza ushirikiano uimarishwe kati ya mkandarasi BCEG kutoka China na wazawa wanaotekeleza mradi huo.

“Sisi viongozi tunapokuja hapa mnaonekana ninyi ni kitu kimoja, lakini kumbe tunapoondoka kunakuwa na division (mgawanyiko) ndani yenu, hiyo haiwezi kukubalika na serikali haiwezi kupenda, huo unaonekana kama ni ubaguzi katika uwajibikaji, kwa hiyo hilo hatuwezi kulikubali.

“Nitoe wito kwenu na nitafuatilia kuona haya ninayoyasema ndiyo yanayofanyika, na msipokuwa mnarekebisha hali hiyo tutaishauri serikali na wenye mamlaka ya mradi huu waone namna nzuri ya kufanya, ni lazima solidarity (mshikamano) yenu iwe kubwa ili mradi uweze kwenda kwa kasi,” amesisitiza RC Mtanda.

Aidha, kiongozi huyo wa mkoa amemtaka mkandarasi kuongeza kasi katika utekelezaji wa mradi huo hata kama serikali haijamlipa fedha zake zote, ili uweze kukamilika kwa wakati.

Pamoja na hayo, RC Mtanda ameitaka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mara ambayo ndio Mshauri wa mradi huo kutekeleza majukumu yake kwa uaminifu na uadilifu kwa manufaa ya Taifa. “Mkifanya kazi hiyo vizuri maana yake mmefanya kazi ya nchi vizuri,” amesema.

Kuhusu changamoto ya fedha, ameahidi kuwa yeye kama kiongozi wa serikali atakwenda kuzungumza na wizara zenye dhamana ya ujenzi na fedha ziweze kumlipa mkandarasi shilingi bilioni 4.9 anazodai, ili kuharakisha utekelezaji wa mradi huo.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe (kulia) akimfafanulia RC Mtanda (mwenye miwani kulia) taarifa ya utekelezaji wa mradi huo.

RC Mtanda amesema faida za mradi huo ni nyingi na mahitaji yake ni makubwa kwa wakazi wa mji wa Musoma na mkoa wa Mara kwa ujumla.

“Meneja wa Uwanja wa Ndege ametueleza kwamba hapa Musoma kuna abiria wengi sana, kwa mwaka kipindi kilichopita ametoa takwimu ni zaidi ya abiria 14,000 wametumia uwanja huu kwa mwaka mmoja kabla uwanja huu haujaanza matengenezo yake. Kwa hiyo uwanja huu una matumizi makubwa sana kwa wananchi wa Musoma,” amesema.

Lakini pia, ameeleza kwamba uwanja huo ni muhimu kutokana na mkoa wa Mara kuwa na utajiri mkubwa wa madini na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, miongoni mwa nyingine lukuki.

“Wafanyabiashara wa madini wangependa kuja kununua madini na kuondoka nayo kwa wakati, wanapenda kuja kutua hapa Musoma kwenda huko Tarime, Nyamongo maeneo ya madini.

“Lakini pia Mara ni mkoa wa utalii, watalii wangependa watue hapa waende Serengeti kwa muda mfupi halafu waweze kuondokea uwanja huu wa Musoma kurudi ambako wametoka. Kwa hiyo upanuzi wa uwanja huu ni tija kubwa sana,” amesisitiza RC Mtanda.

Mkuu huyo wa Mkoa ametumia nafasi hiyo pia kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha shilingi bilioni 35 kwa ajili ya kugharimia utekelezaji wa mradi huo.

“Wizara zinazohusika na menejimenti ya mkoa tunashirikiana na TANROADS na Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kuhakikisha kwamba tunafuatilia fedha zifike kwa wakati ili mradi huu sasa ukamilike kwa wakati, na sisi wana-Musoma tusilazimike kupanda ndege Mwanza na maeneo mengine,” amesema.

Awali, akisoma taarifa ya ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege Musoma, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe amesema utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 50 na unatarajiwa kukamilika baada ya miezi 10 ijayo.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages