NEWS

Monday 17 July 2023

Ujenzi barabara ya lami Mogabiri - Nyamongo wafikia asilimia 20, Mkuu wa Mkoa ataka kusiwepo vikwazoMkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda (kushoto) akisikiliza kutoka kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe, maelezo ya utekelelezaji wa mradi wa ujenzi wa lami barabara ya Mogabiri - Nyamongo alipoutembelea, wiki iliyopita.
-----------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime
--------------------------------------

MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Said Mohamed Mtanda amekagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Tarime – Mugumu (Serengeti) sehemu ya Mogabiri – Nyamongo kwa kiwango cha lami, na kutaka kusiwepo na vikwazo vyovyote vinavyoweza kuchelewesha ujenzi huo.

Katika ziara yake hiyo ya Jumatatu iliyopita, RC Mtanda alifuatana na Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe ambaye pamoja na changamoto nyingine, alisema kuna wananchi wachache waliogoma kuchukua malipo ya fedha ili kupisha uchukuaji wa malighafi za ujenzi wa barabara hiyo.

Kwa mujibu wa Mhandisi Maribe, baadhi ya wananchi wenye maeneo yaliyofanyiwa uthamini na Mthamini wa Serikali wanakataa kupokea malipo yao wakidai kiasi cha malipo hayo ni kidogo licha ya kushirikishwa kikamilifu na kusaini mikataba.

“Kwa kuwa mradi lazima utekelezwe kwa kutumia material (malighafi ) yaliyopo maeneo haya - changamoto kubwa iliyopo ni kwamba Mthamini wa Serikali anakuja anafanya uthamini, watu wanaonesha kiwango cha kulipwa wanasaini mkataba, lakini siku ya kulipwa wanakataa kuwa pesa ni ndogo,” Mhandisi Maribe alimueleza Mkuu huyo wa Mkoa wa Mara.

Kwa upande mwingine, Mhandisi Maribe alisema mvua zilizonyesha wilayani Tarime miezi ya hivi karibuni zimechangia kuathiri maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo.

Akijibu hoja ya wananchi wanaokataa kuchukua malipo ili kupisha uchukuaji wa malighafi za ujenzi, RC Mtanda alisema kuna umuhimu wa viongozi wa serikali kwenda kukutana na kuwaelimisha, ili wasiendelee kuchelewesha utekelezaji wa mradi huo.

“Muhimu ni kwamba hao watu mpange mkutano kama hivi tupotembelea hapa site (eneo la mradi) tunawatembelea na wao tuwaelimishe na tujue kwanini wanachelewesha kazi ya serikali wakati wana contract (mkataba).

“Wakati mwingine tunapowasainisha contract tuweke kipengele kinachombana ili akikiuka makubaliano tuweze kumfikisha kwenye vyombo vingine, kwa sababu contract lazima izibane pande zote mbili.

“Lakini kwanza twende tuwape elimu watu wa namna hiyo, nitamtuma Mkuu wa Wilaya atakwenda atazungumza nao ili wasicheleweshe kazi ya serikali, na kazi hii wajue ni kwa faida yao. Kwa hiyo nafikiri wanahitaji kukaa nao, kuzungumza nao,” alielekeza RC Mtanda.

Wakati huo huo, mkuu huo wa mkoa alimtaka mkandarasi wa mradi huo kuongeza kasi ya ujenzi - licha ya kucheleweshewa sehemu ya malipo ya fedha.

“Nimeona changamoto ya fedha, hazijalipwa kwa wakati, lakini bado kasi nafiki inatakiwa kuongezeka kwa sababu muda wa mkataba unakaribia ku- expire (kuisha).


RC Mtanda (wa pili kushoto) na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara, Mhandisi Maribe (mwenye suruali ya kijivu) wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa barabara ya Mogabiri – Nyamongo kwa kiwango cha lami. Kulia ni wakandarasi wa mradi huo.(Picha zote na Ernest Makanya)

Awali, akisoma taarifa fupi kwa RC Mtanda, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara, Mhandisi Maribe alisema ujenzi wa barabara ya Tarime - Mugumu yenye urefu wa kilomita 87.14 kwa kiwango cha lami unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100.

Alisema lengo la serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, ni kuharakiakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa wilaya za Tarime na Serengeti.

Aliongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama tawala - Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili kuunganisha miji ya Tarime na Mugumu kwa barabara ya lami.

“Barabara hii ni kiungo muhimu kwa wakazi wa Mugumu na Tarime, pia ni kichocheo cha maendeleo ya sekta ya utalii kwenye Hifadhi ya Taifa Serengeti na uchimbaji wa madini katika eneo ya Nyamongo,” alisema Mhandisi Maribe.

Kuhusu ujenzi wa barabara hiyo sehemu ya Mogabiri - Nyamongo yenye urefu wa kilomita 25 itakayounganisha miji ya Tarime na Nyamongo kwa lami, alisema unatekelezwa na kampuni ya kizalendo ya Nyanza Road Works, kwa gharama ya shilingi bilioni 34.662.

Aidha, alimtaja Mhandisi Mshauri anayesimamia ujenzi wa barabara hiyo kuwa ni kampuni ya kizalendo iitwayo Advanced Engineering Solutions Ltd kwa kushirikiana na JMK International Consultants Ltd, kwa gharama ya shilingi bilioni 1.563.

“Utekelezaji wa mradi huu ulianza Julai 8, 2022 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Januari 7, 2024. Muda wa utekelezaji wa mradi ni miezi 18, na muda wa uangalizi (defect liability period) ni miezi 12.

“Kwa ujumla hatua ya utekelezaji wa mradi iliyofikiwa hadi sasa ni asilimia 20 ikilinganishwa na asilimia 30 zilizopangwa kufikiwa kulingana na mpango kazi wa Mkandarasi ulioidhinishwa na Mhandisi Mshauri, hivyo utekelezaji wa mradi upo nyuma kwa asilimia 10,” alisema Mhandisi Maribe.

Alitaja kazi zilizokwisha kufanyika kuwa ni kusafisha eneo la kujenga barabara yenye urefu wa kilomita 14.9 ambayo tayari imefanyika kwa asilimia 96, kuondoa tabaka la juu la udongo kilomita 13.4 (53.6%) na ujenzi wa tabaka la juu G3 kilomita 11.1 (44.4%).

Kazi nyingine zilizofanyika ni ujenzi wa tabaka la udongo G7 kilomita 10.2 (40.8%), ujenzi wa tabaka la udongo G15 kilomita 6.6 (26.4%) na ujenzi tabaka la chini la msingi kilomita 0.3 (1.2%).

Nyingine ni ujenzi wa makalvati madogo 37 (31.4%), makalvati makubwa 10 (40.0%), usimikaji wa mtambo wa kusaga kokoto (100%), usimikaji wa mtambo wa kuchanganya zege (100%) na ujenzi wa kambi ya Mhandisi Mshauri (100%).

Kuhusu ajira, Mhandisi Maribe alisema mradi wa ujenzi wa barabara ya Mogabiri - Nyamongo umezalisha ajira kwa watu 186, ambapo kati ya hao, waajiriwa 176 sawa na asilimia 94.6 ni Watanzania.

Chanzo: SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages