Na Mwandishi wa
Mara Online News
---------------------------
CHAMA Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU
Ltd) kimeshusha tani 31 (sawa na kilo 31,000) za mbegu bora za mahindi aina ya
DK kutoka Kampuni ya Bayer Life Science Tanzania Limited, kwa ajili ya kuuzia wakulima kwa bei nafuu.
Mara Online News ilishuhudia mbegu hizo zikishushwa
kwenye maghala ya WAMACU Ltd yaliyopo eneo la Rebu mjini Tarime, jana.
Kwa mujibu wa Meneja Mkuu (GM) wa WAMACU Ltd, Samwel
Gisiboye, mbegu hizo zitauzwa kwa bei ya shilingi 14,000 kwa mfuko wa kilo
mbili kipindi hiki cha msimu wa vuli.
“Tumeamua kuwaletea wakulima mbegu hizi ili kuwaepusha
kununua zinazotoka nje ya nchi ambazo mara nyingi zinachakachuliwa na
kuwaingiza wakulima hasara.
“Hivyo tunawahimiza wakulima wetu kutumia mbegu hizi
ambazo hutengenezwa hapa nchini na Kampuni ya Bayer iliyoidhinishwa na Serikali
yetu,” alisema GM Gisiboye katika mazungumzo na Mara Online News ofisini kwake,
jana.
Alisema WAMACU Ltd itaendelea kuongeza mbegu nyingi
iwezekanavyo ili kutosheleza mahitaji ya wakulima. “Tunatarajia kuongeza mbegu
hizi hadi kilo 150,000 msimu huu wa vuli,” alisema.
Kwa mujibu wa Kampuni ya Bayer Life Science Tanzania Limited, mbegu bora za mahindi
aina ya DK huzaa mapema, punje zake ni kubwa, hukomaa ndani ya siku 90 hadi 110
na mavuno yake ni magunia 28 hadi 32 kwa ekari moja.
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment