NEWS

Friday 4 August 2023

TACAIDS yaelimisha wananchi Rorya kupinga ukatili wa kijinsia, ubaguzi kwa wanaoishi na VVU




Na Joseph Maunya, Tarime
------------------------------------
 

TUME ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) imeshirikiana na Shirika la AGE-Upgrade kuelimisha wananchi wilayani Rorya kuachana na mila zinazochangia ukatili wa kijinsia na ubaguzi dhidi ya wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU). 

  Mratibu wa masuala ya jinsia kutoka TACAIDS, Judith Luande aliyasema hayo jana wakati wa kampeni ya kuelimisha wakazi wa kata za Tai, Roche na Ikoma madhara ya ukatili wa kijinsia na maambukizi ya VVU katika jamii. 
Judith Luande akitoa elimu wakati wa ziara hiyo

  “Ndugu zangu tuachane na mila zinazoleta ukatili pamoja na kuondoa usawa wa kijinsia katika jamii zetu kwa sababu zinachangia kukwamisha maendeleo kwa kutotoa fursa sawa za kiuchumi kwa wanawake na wanaume. 

  "Lakini pia wale wenzetu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi tusiwanyanyapae, tuwasaidie kupata haki zao za msingi ili waweze kuishi vizuri kama watu wengine katika familia zetu na jamii yote inayotuzunguka," alisema Luande. 
Wananchi wakifuatilia mafunzo

  Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mara, Neema Ibamba aliwashauri wanaume wanaotendewa ukatili na wenza wao kujitokeza kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili wapatiwe msaada, badala ya kukaa kimya, au kufanya maamuzi ya kujidhuru. 

  "Hata wanaume pia wanatendewa ukatili, kwa hiyo tunawaomba na ninyi pia mlete taarifa katika vyombo vya sheria ili tuweze kushughulika na wanawake wanaowatendea ukatili, msinyamaze - hata ninyi pia ni wanadamu," alisema Ibamba. 
Neema Ibamba akizungumza wakati wa ziara hiyo

  Mwenyekiti wa Baraza la watu wanaoishi na VVU wilayani Rorya, Richard Kenyatta Oloo aliahidi kushirikiana na TACAIDS katika mapambano dhidi ya maradhi hayo ili kuokoa kizazi cha sasa na vijavyo. 

  Nao wananchi wa kata hizo waliishukuru TACAIDS kwa ziara hiyo ya kutoa elimu. "Nimefurahishwa na elimu mliyotupatia kuhusu kujilinda, kujikinga na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi pamoja na mambo mbalimbali ya ukatili wa kijinsia," alisema Salu Kema Mapembe, mkazi wa kata ya Tai. 
Sehemu ya washiriki wa mikutano ya ziara hiyo ya TACAIDS

  TACAIDS inashirikiana na AGE-Upgrade katika kampeni ya kuwezesha watu wanaoishi na VVU kimafunzo kwa ajili ya kusaidia kuyafikisha kwenye jamii. 

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages