NEWS

Friday, 29 August 2025

Professor Mwera Foundation kuwapa wanafunzi ofa ya kusoma sekondari, ufundi bure



Mkurugenzi wa Professor Mwera Foundation (PMF), Hezbon Peter Mwera (aliyevaa suti nyeusi), walimu na wanafunzi katika picha ya pamoja wakati wa Mahafali ya Tano ya Darasa la Saba ya Shule ya Msingi Mwera Vision jana Agosti 28, 2025.
---------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime

Uongozi wa Professor Mwera Foundation (PMF) umetangaza ofa ya kuwalipia wahitimu wa Shule ya Awali na Msingi Mwera Vision iliyopo mjini Tarime, mkoani Mara ada ya kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko pamoja na kozi moja ya ufundi kwenye Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime (TVTC).

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa taasisi hiyo - inayomiliki shule hizo na chuo hicho, Hezbon Peter Mwera, wanafunzi watakaonufaika na ofa hiyo ni ambao walisoma chekechea hadi darasa la saba shuleni hapo.

Hezbon alitangaza ofa hiyo wakati wa Mahafali ya Tano ya Darasa la Saba ya Shule ya Msingi Mwera Vision yaliyofanyika shuleni hapo jana, ambapo wanafunzi 12 (wavulana sita na wasichana sita) wanatarajiwa kufanya Mtihani wa Taifa mwezi ujao.


Mgeni rasmi, Mwl Revocatus Baru, akimkabidhi mmoja wa wanafunzi hao cheti cha kuhitimu darasa la saba. Mwenye suti nyeusi ni Mkurugenzi wa PMF, Hezbon Peter Mwera.
----------------------------------------

"Taasisi itakwenda kusimamia karo ya wanafunzi wote pamoja na kozi moja ya ufundi bure kuwaunga mkono wazazi waliosomesha wanafunzi hapa kuanzia chekechea mpaka la saba," alisema Hezbon.

Mkurugenzi huyo wa PMF alitumia nafasi hiyo pia kuwakaribisha wazazi na walezi kupeleka watoto wao katika shule hiyo kwa gharama nafuu.

"Sisi tunajivunia utofauti tulionao, gharama kwetu ni nafuu sana, tunaamini kuwa hatujafika hapa bila kushikwa mkono, hatuangalii kutengeneza faida. Ukiwa mbinafsi Mungu anakunyang’anya ulichonacho ndio maana unaona tunatoa ofa, ikiwemo ya kusomesha vijana wa Tarime bure. Mpaka sasa tumeishasomesha vijana zaidi ya elfu sita," alieleza.


Mkurugenzi wa PMF, walimu na wanafunzi wa darasa la saba katika picha ya pamoja.
----------------------------------------

Kwa upande wake, mgeni rasmi katika mahafali hayo, Mwl Revocatus Baru, aliahidi kuipatia shule hiyo msaada wa kompyuta, huku akihimiza umuhimu wa elimu ya ufundi kwa vitendo.

"Sasa tunataka watoto wanaomaliza shule ya msingi watoke na fani ya ufundi ili iwasidie maishani - hata asipoendelea na masomo,” alisema Baru.

Aidha, alimpongeza Mkurugenzi wa PMF, Hezbon, kwa ubunifu katika shule hiyo na kumwahidi makubwa. “Shule hii tunaenda kuiboresha, tuko tayari kusaidia vitabu vya mtaala mpya. Wazazi tusikose kuleta wanafunzi kwenye shule hizi zenye mkondo wa amali," alisema.

Nao wanafunzi wa shule hiyo, akiwemo Grace Michael, waliahidi kufanya vizuri kwenye mitihani yao na kupata matokeo mazuri wakisema wamefundishwa kwa weledi wa hali ya juu kukuza vipaji vyao na kulelewa kiroho.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages