NEWS

Saturday 30 September 2023

Barrick North Mara yatoa gari la kufuatilia miradi ya CSR kamati mpya ya CDC ikizinduliwa Tarime Vijijini



Rais na CEO wa Barrick, Mark Bristow akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele ufunguo wa gari la kufuatilia miradi ya CSR.
-------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime –
Mara Online News
--------------------------


KAMPUNI ya Barrick imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) gari aina ya Toyota Land Cruiser kwa ajili ya ufuatiliaji wa miradi ya inayoifadhili katika halmashaui hiyo kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR). 

Rais na Mtendaji Mkuu (CEO) wa Barrick, Mark Bristow alikabidhi gari hilo jana Ijumaa kwa viongozi wa halmashauri hiyo na kuomba itunzwe vizuri na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.



“Hili gari ni kwa ajili ya kutusaidia kwenye safari yetu ili kufika tunapohitaji kuwa (destination),” alisema Bristow. 

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Meneja Mkuu (GM) wa Mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko alisema gari hilo litasaidia kuimarisha usimamizi wa miradi ya CSR. 

“Tuna miradi zaidi ya 100 ya CSR, na ili kazi iende sawa tumeona tuwe na gari hili kwa ajili ya ufuatiliaji,” alisema GM Lyambiko. 


Dereva akikagua gari hilo

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele alisema gari hilo ni muhimu katika kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya CSR kutoka Barrick. 

“Tunashukuru Barrick kwa gari hili, litasaidia wataalamu wetu kufika kwenye miradi kwa wakati na miradi kutekelezeka kwa wakati, ili iweze kunufaisha wananchi wetu,” alisema Kanali Mntenjele. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya (DED) ya Tarime, Solomon Shati alisema gari hilo linakuwa chachu ya ufuatiliaji na usimamizi mzuri wa miradi ya CSR. 

Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara umetumia zaidi ya shilingi bilioni saba kugharimia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijami kupitia mpango huo wa CSR katika vijiji vyote 88 vya halmashauri ya Wilaya ya Tarime, ambapo asilimia 70 ya kiasi hicho cha fedha kikienda kwenye vijiji vinavyouzunguka. 

Wakati huo huo, Rais na CEO wa Barrick, Bristow, amezindua Kamati mpya ya Maendeleo ya Jamii (CDC) ya mgodi huo ambayo kwa sasa Mwenyekiti wake mpya ni Diwani wa Kata ya Matongo, Godfrey Kigoye. 


CDC ilianzishwa na Kampuni ya Barrick kwa lengo kuu la kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi wenyeji kutokana na fedha za mpango wake wa CSR. 

Katika hatua nyingine, Bristow amezindua mashindano ya soka ya Kombe la Mahusiano (Mahusiano Cup) yaliyoandaliwa na mgodi wa Barrick North Mara, yenye kaulimbiu inayosema: “Mahusiano Bora kwa Uwekezaji Endelevu”. 


Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mashindano hayo, GM wa Mgodi wa Barrick North Mara, Lyambiko alisema: “Mahusiano Cup inatuleta pamoja na kuibua vipaji.” 

GM Lyambiko alidokeza kuwa mpango wa ujenzi wa uwanja wa soka wa kisasa unaedelea vizuri. 

“Tupo kwenye mchakato wa kupata uwanja wa kisasa na tunaendelea na upembuzi yakinifu,” alisema Lyambiko na kutumia nafasi hiyo pia kuwaomba wananchi wanaoishi jirani na mgodi huo kusaidia kukemea vitendo vya uvamizi wa mgodi vinavyofanywa na baadhi ya makundi ya watu. 

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Mntenjele, aliushukuru mgodi huo kwa kuandaa mashindano hayo, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuirimarisha mahusiano kati ya mgodi na jamii kwa faida ya pande zote mbili. 

Katika hafla hiyo, viongozi wa mila kutoka koo zote za kabila la Wakurya walimpatia Rais na CEO wa Barrick, Bristow, zawadi ya beberu la mbuzi ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa kampuni hiyo kwa maendeleo ya wananchi wa Tarime. 


#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages