NEWS

Saturday 23 September 2023

DC Mashinji: Faru wanapaisha idadi ya watalii Hifadhi ya Taifa SerengetiMkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dkt Vincent Mashinji akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Faru Duniani yaliyofanyika kiwilaya katika eneo la Fort Ikoma ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti, jana Septemba 22, 2023.
------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Serengeti
-----------------------------------------


MKUU wa Wilaya (DC) ya Serengeti, Dkt Vincent Mashinji amesema uwepo wa Faru katika Hifadhi ya Taifa Serengeti, umechangia kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo. 

Ongezeko la wanyamapori hao ambao ni kivutio kwa watalii wa ndani na nje, limechangiwa na juhudi kubwa za ulinzi zinazofanywa na maafisa na askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), waliojitolea kwa jasho na damu kuhakikisha wanyama hao adimu wanaendelea kuwepo. 

DC Mashinji aliyasema hayo jana Septemba 22, 2023 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Faru Duniani yaliyofanyika Fort Ikoma ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti, ambapo wadau mbalimbali walishiriki mbio fupi. 


Faru ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti

“Nimefurahi kuambiwa kuwa wanyama hawa adimu idadi yao inaongezeka mwaka hadi mwaka, ongezeko la wanyama hawa limeendelea kuvuta watalii wengi sana wa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Niwahakikishie kama Mkuu wa Wilaya hii ya Serengeti, nitashirikiana na TANAPA kukilinda kizazi hiki cha Faru kisitoweke,” alisema. 

Aidha, DC Mashinji aliwapongeza maafisa na askari kwa kuwatunza Faru hao, na kuwaomba kushirikiana na jamii inayozunguka Hifadhi ya Taifa Serengeti, iweze kutoa taarifa pale inapowaona wakiwa nje ya maeneo ya asili, ili wasiuawe na majangili wasioutakia mema uhifadhi. Hata hivyo, DC huyo aliwashauri TANAPA kuangalia uwezekano wa Faru kuongezwa na kuhifadhiwa katika Hifadhi za Taifa Burigi-Chato, Arusha na Nyerere ili watalii wenye shauku ya kuwaona wawe na machaguo mengi zaidi badala ya Serengeti na Mkomazi kama ilivyo sasa. 

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Albert Mziray akimkaribisha mkuu wa wilaya hiyo, alitoa pongezi kwa wawekezaji kutokana na mchango wao mkubwa katika kufanikisha kazi ya uhifadhi na utunzaji wa Faru. 

“Nichukue nafasi hii kuwapongeza Frankfurt, WWF, Friends of Serengeti na majirani zetu TAWA kwa kuja kwenye maadhimisho haya. Pia kwa mchango mkubwa mnaoutoa katika kufanikisha utunzaji wa Faru hawa na shughuli zote za uhifadhi kwa ujumla,” alisema DC Mashinji. Akifafanua kwa niaba ya Mratibu wa Faru Taifa, Mhifadhi Mkuu Emmanuel Kaaya alisisitiza kuendeleza jitihada za kuimarisha ulinzi wa Faru, ili kutimiza malengo ya uhifadhi wa Faru, hasa katika kutekeleza mkakati wa Faru Taifa. 

“Tutawapa tuzo washindi wa mbio za asubuhi pamoja na watumishi waliojitolea usiku na mchana kuwahifadhi Faru kwa mwaka huu wa 2023, tunafanya hivi ili kuenzi na kuheshimu mchango wenu,” alisema Kaaya. 


Maadhimisho hayo ya Siku ya Faru Duniani yaliyofanyika katika Hifadhi ya Taifa Serengeti, yalitanguliwa na mbio zilizohamasisha utunzaji wa Faru na kuongozwa na kaulimbiu inayosema “Tuwalinde Faru dhidi ya ujangili ili tuongeze idadi yao.”

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages