NEWS

Wednesday 20 September 2023

Makamu Mwenyekiti, Wenyeviti wa Kamati za Kudumu watetea nafasi zao, madiwani wawapongeza Mwenyekiti Kiles, DED Shati Halmashauri ya Wilaya Tarime Vijijini



Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Simion Kiles Samwel (aliyesimama) akihutubia kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo Nyamwaga leo Jumatano. Kushoto ni Makamu wake, Petro Kurate na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Solomon Shati.
---------------------------------------------------

Na Christopher Gamaina, Tarime –
Mara Online News
-------------------------- 


MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) wamechagua Makamu Mwenyekiti na Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Halmashauri hiyo, ambapo wote waliokuwa wanashikilia nafasi hizo wamefanikiwa kuzitetea. 

Uchaguzi huo umefanyika wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani hao kilichofanyika Nyamwaga leo Jumatano, kikiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Simion Kiles Samwel. 


Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kikaoni leo Jumatano

Katika uchaguzi huo, Diwani wa Kata ya Mwema, Petro Kurate amefanikiwa kutetea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri. 

Diwani wa Kata ya Manga, Steven Gibai amechaguliwa kuendelea na nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Maji (Maendeleo ya Jamii), huku Diwani wa Kata ya Matongo, Godfrey Kegoye naye akitetea nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira, Ujenzi na Uchumi. 

Naye Diwani wa Kata ya Pemba, Ngocho Wangwe amefanikiwa kuchaguliwa kuendelea na nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili na Ukimwi, huku Kamati ya Fedha, Mipango na Utawala ikiendelea kuwa chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Halmashauri, Kiles, kwa mujibu wa sharia na kanuni. 


Diwani Kurate (aliyesimama) akiwashukuru madiwani kwa kumchagua tena kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime. (Picha zote na Mara Online News)

Katika hatua nyingine, madiwani hao wamempongeza Mwenyekiti Kiles na Mkurugenzi Mtendaji (DED), Solomon Shati kwa usimamizi mzuri wa shughuli za halmashauri hiyo. 

Kwa upande wake, DED Shati amewapongeza madiwani hao na watumishi wa halmashauri hiyo kwa ushirikiano mzuri waliompa hadi kuiwezesha kufikia mafanikio mbalimbali. 

“Tuendelee kushirikiana na kusimamia miradi ya maendeleo ya wananchi ili kuhakikisha inatekelezwa na kukamilika kwa wakati na value for money (thamani ya fedha) ionekane,” amesema DED Shati. 

Akifunga kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Kiles ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyakonga, amewataka madiwani na watumishi kuongeza uchapaji kazi na kujituma ili kuiwezesha kupata mafanikio ya kishindo zaidi katika mwaka wa fedha 2023/2024. 

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages