NEWS

Wednesday 27 September 2023

Walimu, wanafunzi wapongeza Right to Play, AICT kuhamasisha elimu kwa mtoto wa kike Tarime Vijijini



Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Keisangora, Simon Magacha (kulia) akikabidhi kombe kwa washindi wa tamasha la michezo lililoandaliwa na Shirika la Right to Play kwa kushirikiana na AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Keisangora wilayani Tarime, jana Jumanne.
-------------------------------------------------

Na Joseph Maunya, Tarime –
Mara Online News
-------------------------- 


WALIMU na wanafunzi wa shule za msingi Nyamerama na Keisangora zilizopo kata ya Nyamwaga katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), wameeleza kufurahishwa na hamasa ya elimu kwa mtato wa kike inayotolewa na Shirika la Kimataifa la Right to Play kwa kushirikiana na Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe. 

Walitoa shukurani hizo jana Jumanne wakati wa tamasha la michezo mbalimbali kwa wanafunzi wa shule hizo, lililoandaliwa na Right to Play katika viwanja vya Shule ya Msingi Keisangora, ambapo pia walimu na wanafunzi walijengewa uwezo wa kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo. 
Mchezo wa kuvuta kamba

Mwanafunzi wa darasa la sita kutoka Shule ya Msingi Nyamerama, Irene Medison aliwashukuru Right to Play akisema mbali na kuhamasisha elimu kwa mtoto wa kike, fursa hiyo imewasaidia kuibua na kukuza vipaji vyao vya michezo. 

Nelson Mwita, mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Keisangora alisema “Kwa leo nimejifunza michezo mbalimbali, lakini pia nawashukuru sana Right to Play kwa kuwa kupitia wao nimejifunza kusoma, mfano nilipokuwa darasa la pili nilikuwa sijui kusoma wala kuandika, ila sasa hivi najua.” 
Wanafunzi wakifurahia ushindi

Kwa upande wao, walimu wa shule hizo walisema mbali na kusaidia kuinua taaluma kwa wanafunzi, Shirika la Right to Play na AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe wanawajengea walimu uwezo wa kutekeleza majukumu yao ya ufundishaji. 

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Keisangora, Simon Magacha ambaye alikuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo la michezo alisema “Nawapongeza Right to Play na AICT maana wanawezesha walimu na wanafunzi. Pia sisi kama Serikali tutaendelea kuwakaribisha na kufanya nao kazi.” 


Afisa Mradi kutoka AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Rebeca Bugota akizungumza wakati wa tamasha hilo.

Afisa Mradi kutoka AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Rebeca Bugota alisema wanashirikiana na Right to Play kuendesha shughuli zao katika kata za Nyamwaga, Itiryo na Nyansincha wilayani Tarime, wakijikita katika kuhamasisha elimu kwa mtoto wa kike na iliyo jumuishi, sambamba na kuwajengea vijana na walimu uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali. 

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages