NEWS

Monday 23 October 2023

Makonda Katibu mpya wa NEC ya CCM, Sophia Mjema naye ateuliwa kuwa Mshauri wa RaisPaul Makonda

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
----------------------------------------
 

ALIYEWAHI kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika Serikali ya Awamu ya Tano, Paul Makonda, ameteuliwa kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Itikadi na Uenezi. 

Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ilifanya uteuzi huo wakati wa kikeo chake maalum, kilichofanyika jijini Dodoma, jana Jumapili. 

Kwa uteuzi huo, Makonda anachukua nafasi iliyokuwa ikitumikiwa na Sophia Mjema ambaye jana hiyo hiyo aliteuliwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa Mshauri wa Rais masuala ya Wanawake na Makundi Maalum. 

Sophia Mjema

Naye Rabia Abdallah Hamid aliteuliwa kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), nafasi iliyokuwa ikitumikiwa na Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki. 

Katika kikao hicho, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa chini ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, pia iliridhia kwa kauli moja na kuielekeza Serikali kuendelea na hatua ya utiaji saini mikataba ya uendelezaji na uwekezaji wa bandari. 

Pia Halmashauri Kuu ya CCM Taifa katika kikao hicho, ilizipongeza Serikali zake zote mbili; Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar - chini ya Rais Dkt Hussein Ali Mwinyi, kwa kazi kubwa na nzuri ya kuendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 - 2025. 

Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA 
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages