NEWS

Friday 6 October 2023

Maryo Sekondari yasherehekea Mahafali ya Kwanza ikijivunia mafanikio kemkem, Mkurugenzi wa HSF ahimiza malezi bora kwa watoto



Mkurugenzi wa Taasisi ya HSF, Emmyliana Range akizungumza wakati wa Mahafali ya Kwanza ya Wahitimu wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Maryo, jana Alhamisi.
---------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Nyamongo –
Mara Online News
--------------------------


SHULE ya Sekondari Maryo iliyopo Nyamongo wilayani Tarime, Mara imesherehekea Mahafali ya Kwanza ya Wahitimu wa Kidato cha Nne, huku ikijivunia mafanikio ya kitaaluma na huduma bora kwa wanafunzi na walimu wake. 

Wakisoma risala kwa mgeni rasmi katika mahafali yao yaliyofanyika shuleni hapo jana Alhamisi, wahitimu hao walitaja mafanikio ya kitaaluma kuwa ni pamoja na kupata ufaulu wa daraja A (Division One) katika Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Pili kwa miaka miwili mfululizo (2021 na 2022). 

Aidha, walitaja huduma bora zitolewazo kwa wanafunzi na walimu shuleni hapo kuwa ni maji safi ya bomba, chakula bora, umeme, majengo ya kisasa yakiwemo mabweni, madarasa, maabara, bwalo la chakula na nyumba za walimu.


Mkurugenzi Emmyliana akikabidhi cheti kwa mhitimu wa kidato cha nne

Akizungumza katika mahafali hayo, Mkurugenzi wa Health and Safe Delivery Baby Foundation (HSF), Emmyliana Range aliwahimiza wazazi kuhakikisha wahitimu hao watakaporudi nyumbani wanapata malezi bora ili waendelee kuwa kioo cha jamii kwa nidhamu na maadili mema.

"Wazazi lindeni watoto wenu, msiwapeleke kuishi kwa ndugu zenu, kaeni na watoto wenu nyumbani mkiwapatia malezi bora," alisisitiza Emmyliana ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Lumry Company, Lucy Marwa Ryoba kama mgeni rasmi kwenye mahafali hayo.


Wahitimu wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Maryo

Katika hatua nyingine, Emmyliana aliwasilisha mchango wa shilingi milioni tano taslimu uliotolewa na Mkurugenzi Lucy kuchangia ujenzi wa chumba cha masomo ya kompyuta shuleni hapo. 

Pia wadau wengine kutoka taasisi mbalimbali na wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo waliunga mkono juhudi hizo kwa michango ya fedha na vifaa vya ujenzi kupitia harambee ndogo iliyoongozwa na Mkurugenzi Emmyliana wakati wa mahafali hayo yaliyofana kwa aina yake. 

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages