Pamba shambani
------------------------------------------
WAKULIMA wa pamba wamependekeza mambo matatu yanayoweza kuwaondolea tatizo la kushuka kwa bei ya zao hilo la biashara.
Wakizungumza na Gazeti la Sauti ya Mara kwa nyakati tofauti mkoani Mara hivi karibuni, wakulima hao walisema ili kuimarisha bei ya pamba itakayokuwa na tija kwao, kwanza Serikali irejeshe utaratibu wa kuwashirikisha kwenye vikao vya kupanga bei ya zao hilo.
Pili, Serikali iangalie uwezekano wa kufufua viwanda vya nguo vilivyokufa na kujenga vingine, na tatu, ipunguze tozo kwa wafanyabiashara ya pamba.
“Wakulima tushirikishwe kwenye vikao vya kupanga bei ya pamba, Serikali yetu ifufue viwanda vya nguo na kuongeza vipya nchini ili pamba tunayozalisha iuzwe hapa hapa nchini ndio bei itapanda. Lakini pia Serikali ipunguze ushuru angalau mnunuzi ainunue na kuisafirisha kwa tija, maana tozo zinakuwa nyingi,” alisema Mageta Magabe, mkulima bora wa pamba kutoka kijiji cha Gusuhi kilichopo kata ya Nyambureti wilayani Serengeti.
Mkulima wa pamba kutoka wilayani Musoma ambaye aliomba kutotajwa jina alisema: “Wakulima tumewekwa pembeni kwenye suala hili la kupanga bei, yaani kulima ulime na kupambana mwenyewe halafu mtu mwingine anakupangia bei, hii sio sawa kabisa.”
Mwenyekiti wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) Mkoa wa Mara, Madaraka Mashauri alisema Tanzania haina sababu ya kuendelea kuagiza nguo kutoka nje ya nchi wakati ina uwezo wa kujenga viwanda vya ndani na hata wataalamu wa kuviendesha wapo.
“Tuwe na viwanda vya ndani na vifanye kazi. Hatuna sababu ya kuendelea kununua mitumba ya wazungu wakati tuna uwezo wa kuzalisha pamba na kuwa na viwanda vyetu. Kama ni wataalamu tunao na hata kama kuna kinachokosekana tutajifunza. Hii ya kutegemea kwa asilimia 100 nguo kutoka Ulaya hapana.
“Kuendelea kuagiza nguo kutoka nje ya nchi ni aibu kubwa. Serikali ilivalie njuga suala hili, tuwe na viwanda vyetu, tununue khanga na shuka za pamba yetu,” alisema Madaraka na kuhoji: “Kwanini hili suala la kuwa na viwanda vya nguo wabunge wetu hawalipi msukumo, wameridhika tu pamba inashuka bei?”
Kwa upande mwingine, wakulima hao waliiomba Serikali kutupia macho taswira ya biashara ya pamba kuhodhiwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa kwani wamekuwa wakitumia nyadhifa zao kukandamiza wakulima kwenye bei ya zao hilo.
La sivyo, wakulima hao walisema nchi itarajie kushuhudia kushuka kwa mavuno ya pamba kutokana na wengi kukipa kisogo kilimo hicho.
“Mfano mkulima aliyekuwa na ekari tano za kulima pamba amerudi nyuma - analima ekari mbili tu. Kwa ujumla wakulima wengi sasa hivi wamekata tamaa, wamevunjika moyo - wameamua kuachana na pamba, wamehamia kwenye mazao ya mahindi na alizeti,” alisema Mageta.
Gazeti la Sauti ya Mara linaendelea na juhudi za kuwapata viongozi wenye dhamana ya zao la pamba ili waweze kutoa ufafanuzi juu ya kilio hicho cha wakulima.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment